Agizo la DC wa Singida kwa wananchi kuhusu waharifu wa Kibiti, Pwani

439
0
Share:
Mkuu wa wilaya ya Singida, Elias Tarimo, amewaagiza wakazi wa wilaya hiyo kuwafichua wageni wasioeleweka kwa madai baadhi ya wauaji kutoka Kibiti mkoani Pwani, wameaanza kukimbilia wilayani humo kwa lengo la kujificha. 

Wilaya ya Singida ina halmashauri ya wilaya ya Singida yenye makao yake makuu ya muda katika kijiji cha Ilongero na halmashauri ya manispaa.

DC Tarimo ametoa agizo hilo juzi mbele ya kikao cha kawaida cha madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Singida.

Akilijengea nguvu agizo lake hilo, alisema hivi karibuni jeshi la polisi liliuwa mwanaume mmoja anayeaminika ametokea Kibiti, wakati wa majibizano ya risasi kati yake na Polisi.

“Wakati tunafanya operation ya kuwahamisha wavamizi haramu kwenye hifadhi ya msitu wa Magori, raia wema walitupa taarifa kwamba nyumbani kwa wananchi mmoja (jina tunalo), kuna mgeni ambaye wanamtilia shaka kwamba atakuwa ni kutoka kikundi kinachouwa wananchi wasio na hati huko Kibiti,” alifafanua.

Akifafanua zaidi, alisema baada ya taarifa hiyo, Polisi waliizingira nyumba hiyo na mgeni huyo alipoombwa kujisalimisha na atoke nje, aligoma. 

“Baada ya kugoma, bomu la machozi lilipigwa ndani ya nyumba hiyo kitendo kilichosababisha atokee dirishani huku akifyetua risasi. Risasi moja ilipiga kifuani kwa polisi mmoja lakini alinusurika kufa, kutokana na kuvaa kinga dhidi ya risasi. Ni chechetu ndizo zilizomjeruhi kwenye shavu,” alifafanua zaidi. 

Alisema kutokana na tukio hilo,wakazi wa wilaya ya Singida wanapaswa kuwa makini na ujio wo wote wa wageni wasioeleweka. Wakimtilia shaka mgeni yoyote, watoe taarifa haraka kwa viongozi wao au kwenye kituo cha polisi kilicho karibu. 

“Tusiruhusu wilaya yetu ikageuzwa kuwa kitovu cha uhalifu au maficho ya watu wenye harufu ya vitendo vya ugaidi.Nasisitiza tulinde wilaya yetu, mkoa wetu na nchi yetu kwa ujumla ili amani na utulivu uendelee kudumu,” alisema Tarimo.

Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya,aliagiza mabango yote ya matangazo ya tiba asilia, yang’olewe na kuharibiwa. 

Amesema baadhi ya waganga wa madawa asili na wanajihusisha na vitendo vya ramli chonganishi ambazo zina madhara makubwa ikiwemo kuchangia vifo.

“Kuna tukio la kutisha limetokea katika halmashauri ya wilaya ya Singida hivi karibuni. Hawa wapiga ramli chonganishi walienda kwenye mji moja na kudai mtoto mdogo aliyekuwa mgonjwa si binadamu ni jini,” alisema na kuongeza.

“Baada ya hapo  akawashawishi wazazi wa mtoto huyo, wamchome moto. ili aweze kubadilika na kuwa binadamu. Mtoto alichomwa moto na kuwa majivu na kuacha vilio na simazi kwa familia.”

Na Nathaniel Limu, Singida

Share:

Leave a reply