Ajali barabarani zapungua kwa 45%, vifo navyo vyashuka kwa 19.6%

594
0
Share:

Vifo vitokanavyo na ajali za barabarani vimepungua, ambapo vya ajali za magari vimepungua kutoka 1,286 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei, 2016 hadi 1,034 kipindi kama hicho mwaka huu, pungufu ya vifo 252 sawa na asilimia 19.6.

Hali kadhalika, vifo vitokanavyo na ajali za pikipiki vimepungua kutoka 347 katika kipindi cha Mwezi Januari hadi Mei, 2016 na kufikia 302 kipindi kama hicho mwaka huu, sawa na pungufu ya vifo 45 iliyo sawa na 13%. 

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam, na Kaimu Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Fortunatus Muslimu wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema ajali za barabarani zimepungua kwa asilimia 42 kwa upande wa magari, na 45% za pikipiki. 

“Ajali za magari zimepungua kutoka 4,177 hadi 2,411 sawa na asilimia 42.3, na za pikipiki zimepungua kutoka 1,110 hadi 607 tofauti ya 503 sawa na 45.3%. Majeruhi ajali za pikipiki wamepungua kwa 52.1% kutoka 950 hadi 455, na upande wa magari majeruhi wamepungua kwa 41% kutoka 3,882 hadi 2,291,” amesema.    

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea na ukamataji na kuwachukulia hatua madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, pamoja na kujenga utii wa sheria bila shuruti kwa madereva ili kuzia ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu.

Pia amewataka askari kuacha kufanya kazi kwa mazoea, bali wafanye kazi kwa nidhamu na maadili ya Jeshi la Polisi ikiwemo kutochukua rushwa kutoa kwa madereva wenye makosa kwa lengo la kutowapa adhabu.

Na Regina Mkonde  

Share:

Leave a reply