Ajali yaua wawili Ikungi, Singida

1364
0
Share:

Watu wawili wamefariki dunia papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Land Cruiser kuacha barabara na kuligonga basi la kampuni ya Taowa Coach, ajali hiyo imetokea leo katika eneo la kijiji cha Kideka wilaya ya Ikungi, Singida.

Ajali hiyo imehusisha Toyota Land Cruiser T.862 DJW lililokuwa likitokea Dar es Salaam likienda Mwanza na basi la kampuni ya Taowa coach ltd ya Dar es Salaam T.159 CWH.

 Ajali hiyo imetokea leo Novemba 11 katika eneo la kijiji cha Kideka kata ya Puma wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio,kaimu kamanda Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Isaya Mbughi, alisema miili ya abiria hao wa Toyota Land Cruiser ambao majina yao wala makazi yao bado hayajulikana, imehifadhiwa katika hospitali ya misioni Puma.

 Mbughi amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa kuna kila ya dalili dereva wa Toyota Land Cruiser alikuwa amelala, na hivyo gari lilihama kutoka upande wa kushoto na kwenda kulia.

“Dereva wa basi la Taowa amejitahidi mno kukwepa gari hilo ndogo, lakini ilishindikana na hivyo kuingia uvunguni mwa basi. Kwa wakati huo, basi lilihama upande wake wa kulia na kwenda nje ya barabara,lakini lilifuatwa huko huko,” alisema kaimu kamanda huyo.

Kaimu kamanda huyo, alisema konda wa basi hilo, amevunjika mkono,na mtoto mmoja mwenye umri kati ya miaka sita na saba, naye amejeruhiwa vibaya. Mtoto  wakati wa ajali alikuwa amelala. Abiria hao wamelazwa katika hospitali ya misheni ya Puma.

Kwa upande wa dereva wa basi,Sodobi Abdalah mkazi wa jijini Dar-es-salaam,alisema  alifanya  juhudi kubwa kukwepa gari hilo ndogo, lakini likawa linaendelea  kuja upande wake,na kushitukia lipo uvunguni mwa basi.

 Abiria wa basi hilo na dereva wa magari ya IT, Joseph Chale, licha ya kumpongeza dereva wa basi, alisema dereva huyo aliwatangazia abiria kuwa kuna gari ndogo imehama barabara na linakuja upande wao.

“Kwa uzoezi wangu wa uderava wa muda mrefu, kwa vyo vyote dereva waToyota Land Cruiser, alikuwa amelala.Pengine alipozinduka na gari lake lipo kwenye mwendo kasi, alishindwa kulimudu,” alisema.

Na Nathaniel Limu, Ikungi
Share:

Leave a reply