Aliyemuua mpenzi wake kwa wivu akamatwa

303
0
Share:

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Machi 31, 2017 limemkamata mtuhumiwa wa mauaji anayefahamika kwa jina la Msuguri David Sylvester (29) ambaye anatuhumiwa kumuua kwa kumchinja aliyekuwa mpenzi wake Samira Masoud na kisha mwili wake kuuweka katika jaba la maji.

Wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Aprili 5, 2017 jijini Dar es Slaam Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Siro ameeleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa alikiri kufanya mauaji hayo mnamo Machi 7, 2017 maeneo ya Kibamba na kutaja sababu ya kufanya tukio hilo kuwa ni wivu wa kimapenzi.

“Mtuhumiwa huyo alikamatwa maeneo ya Sinza Shekilango baada ya ufuatiliaji wa taarifa ya tukio hilo kufanyika, katika mahojiano mtuhumiwa huyo alikiri kufanya mauaji kwa sababu ya wivu wa kimapenzi baada ya kumfumania marehemu chumbani na mwanaume mwingine ambaye hata hivyo mwanaume huyo alifanikiwa kutoroka,” amesema.

Amesema awali mtuhumiwa huyo aliwatumia ndugu wa marehemu ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutumia namba ya simu ya marehemu ukisema “Nendeni mkachukue maiti ya ndugu yenu itaozea ndani”. Hata hivyo, amesema upelelezi bado unaendelea na kwamba utakapo kamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Na Regina Mkonde  

Share:

Leave a reply