“Asilimia 60 ya wanawake wanaishi katika hali ya umasikini uliokithiri”- TNGP

368
0
Share:

Asilimia 60 ya wanawake nchini wanaishi katika hali ya umasikini uliokithiri huku maeneo ya mijini wanawake wanaoishi katika umasikini ni 4% wakati maeneo ya kijijini ni 33%.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Clencensia Shule katika Tamasha la 14 la Jinsia, lililokutanisha wanaharakati na wadau mbalimbali wa masuala ya haki za kijinsia.

“Sababu ya wanawake wengi wa vijijini kuwa masikini ni miundombinu hafifu ya maendeleo katika maeneo ya mijini. Pia kwa mujibu wa takwimu ya Wizara ya Afya asilimia 40 ya wanawake hunyanyaswa. Tamasha hili limelenga kufichua changamoto na unyanyasaji unaowakabili wanawake ikiwemo uwakilishi wa kisiasa, uchumi na kwenye nafasi za ajira. Kutokana na changamoto hizo, tamasha hili litajadili mikakati ya pamoja ya kumkomboa mwanamke kiuchumi,” amesema.

Akizungumza wakati akifungua tamasha hilo, Makamu wa Rais Mama Samoa Suluhu, amesema serikali inaendelea na jitihada za kupunguza umasikini ili kumkomboa mwanamke kiuchumi, na kuwataka wadau mbalimbali na sekta binafsi kuiunga mkono serikali katika kuondoa umasikini maeneo ya vijijini hasa kwa wanawake.

Aidha, Mama Samia ameipongeza TGNP kwa kuandaa tamasha hilo kwa kuwa linalenga kujadili changamoto zinazowakabili wanawake sambamba na kuibua mikakati mipya ya kuondoa changamoto hizo ikiwemo ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Sihaba Nkinga amesema Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi, imeanzisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake katika mikoa 23.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi Msaidizi wa UNFPA Christina Kwayu amesema tamasha hilo ni sehemu ya kuwakutanisha wanawake kwenye kujadili mafanikio na changamoto zao na kuahidi kwamba shirika la UNFPA litaendelea kufadhili tamasha hilo pamoja na harakati nyingine za kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake.

Tamasha la hilo Kijinsia limeandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na asasi za kiraia zinazotetea haki za wanawake. Tamasha hilo kwa mwaka huu limebeba kauli mbiu ya “Mageuzi ya Mifumo Kandamizi kwa Usawa wa Jinsia na Maendeleo Endelevu”

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply