Asilimia 95 ya kina mama wajawazito hufikiwa na huduma ya kupima VVU

226
0
Share:

Asilimia 95 ya kina mama wajawazito hufikiwa na huduma ya kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) ili kuweza kujifungua salama watoto ambao hawana hatari ya kupata maambukizi hayo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji Wa Shirika La Umoja Wa Mataifa La Mpango Wa Ukimwi Duniani (Unaids) Bw. Michael Sidibe wakati alipotembelea ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es salaam leo.

“Hata hivyo asilimia 90 ya walio na maambukizi wamepata dawa za ARV hii imepelekea maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto kupungua katika asilimia 21 mwaka 2009 hadi 7.6 mwaka 2015,” alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy alisisitiza kuwa tunaweka nguvu zaidi kwa vijana na hasa wa kike na vijana walio katika makundi maalum yenye hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa VVU.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano zidi ya UKIMWI ili kufikia malengo ya kutokomeza janga hilo la kiafya katika jamii ifikapo mwaka 2030 kwani maambukizi yamepungua toka asilimia 7.1 mwaka 2007/8 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2011/12.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wa Shirika La Umoja Wa Mataifa La Mpango Wa Ukimwi Duniani (Unaids) Bw. Michael Sidibe amesema kuwa wafadhili wanachangia sehemu kubwa ya muitikio wa mapambano ya UKIMWI hivyo UNAIDS wako tayari kusaidia katika kuandaa mpango endelevu ili kuhakikisha Fedha za wafadhili zikipungua huduma ziendelee.

Aidha Bw. Sidibe amesema kuwa Shirika la UNAIDS limeanzisha mpango wa kuwezesha nchi za Afrika kuwa na wahudumu wa afya ngazi ya Jamii ambao watasaidia kuboresha mfumo mzima wa Sekta ya Afya.

Mbali na hayo Bw. Sidibe ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika mapambano ya UKIMWI nchini, hususani kuweza kufikia takribani Waathirika 935,228 wanaotumia dawa za ARV ifikapo Juni 2017.

Share:

Leave a reply