Bajeti yatajwa kuwa sababu ya filamu za ndani kukosa viwango

456
0
Share:

Ukosefu wa bajeti ya kutosha na ubunifu katika uandishi wa stori, umetajwa kuwa sababu ya filamu nyingi za hapa nchini kukosa ubora na viwango vinavyohitajika.

Hayo yamebainishwa leo Mei 19, 2017 jijini Dar es Salaam na Meneja wa Tamasha la Ziff, Daniel Nyalusi, ambaye amesema soko la filamu za bongo linakua licha ya uzalishaji wake kupungua.

“Soko la filamu linakua na zinaanza kuwa nzuri, lakini wingi wa uzalishaji umepungua. Ukosefu wa bajeti unapelekea wataarishaji kushindwa kutengeneza filamu zenye ubora na viwango vya kimataifa. Pia ukosefu wa ubunifu wakati wa uandishi wa stori nako pia kuna sababisha filamu zetu kukosa ubora,” amesema na kuongeza.

“Watunzi wetu wanaona lazima watunge stori zinazohusu mapenzi ndio zitanunulika, inabidi wabadilike namna ya uandishi pia tukubali kuongeza elimu na kuzitengeza filamu kulingana na bajeti iliyopo. Angalie filamu ya Kiumeni, ni ya bongo movie lakini ina stori tofauti sababu ya ubunifu wa hali ya juu uliotumika.” 

Amesema ili kuondoa ukata wa fedha za kutengenezea filamu zilizo bora, wasanii inabidi wawashawishi wadhamini mbalimbali kudhamini filamu zao kama zinavyofanya nchi zilizoendelea.

“Kwenye filamu unakuta msanii anakunywa bia ya safari, anaitangaza ila watengenezaji bia hiyo hawawalipi. Lakini nchi za wenzetu wasanii wanatumia filamu kutangaza bidhaa zao. Lazima wakubalia kuanza tabia ya kushawishi wadhamini katika filamu zetu,” amesema.

 Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply