Balozi Seif Ali Iddi awapa somo vijana kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar

432
0
Share:

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema ili taifa lisonge mbele linawategemea vijana  wakati wote na wakiwa na jukumu la kuhakikisha linasimamia na kumaliza vitendo vyote viovu ambavyo vinawakabili wananchi.

 

Alisema Serikali zote mbili ile na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na iIe ya Mapinduzi ya Zanzibar zinataka kuona  Vijana wake wanakuwa Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.

 

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akifunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964  katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

 

Alisema vijana ndio warithi wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar dhana iliyoanzishwa  na muasisi wa Mapinduzi hayo Mzee Abeid Amani Karume wana wajibu wa  kusimamia vita vya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa wanawake na watoto,  uonevu  pamoja na ufisadi.

 

Balozi Seif alinukuu maneno ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yaliyosema maana halisi ya Mapinduzi daima sio kupindua watu bali ni kuondoa matendo mabaya katika jamii na kusimamia haki na mazuri yote.

 

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuondoa matendo yote maovu ikiwemo uzembe, uonevu na ubaguzi mambo yanarejesha nyuma au kukwamisha juhudi za Taifa  za kuleta Maendeleo ya Umma.

 

Akizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili Vijana hasa  ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likizikumba nchi nyingi duniani, Balozi Seif alisema takwimu za kimataifa zinathibitisha wazi kwamba zaidi ya vijana Zaidi ya milioni 73 wanakadiriwa kuwa hawana ajira.

 

Alisema kwa bahati mbaya mara nyingi changamoto hii ya ukosefu wa ajira kwa Vijana huhusishwa kuwa ndio chanzo cha vitendo viovu vinavyofanywa na Vijana katika Mataifa mbali mbali Duniani.

 

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Mipango imara ya kukabiliana na changamoto hiyo  hali inayobainisha kuwa sio nzuri na jamii imekuwa ikishuhudia nafasi moja ya ajira nchini kugombewa  na vijana zaidi ya 20.

 

Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) hufanyika ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo yamekuwa yakihusisha vijana na kwa mwaka huu vijana 400 wameshiriki matembezi katika Kijiji cha Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja na kumalizikia Afisi Kuu ya CCM  Kisiwanduzi.

Share:

Leave a reply