Barabara ya Morogoro –Kisaki kujengwa kwa lami

600
0
Share:

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani amesema kuwa serikali itajenga barabara ya Morogoro hadi Kisaki KM 133 Kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika na wananchi kuweza kuitumia kipindi chote cha mwaka.

Mhandisi Ngonyani amesema hayo mara baada ya kukagua barabara hiyo inayounganisha wilaya ya Morogoro Mjini na Morogoro Vijijini ambambo amesisitiza kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani.

Amefafanua  kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanzia Morogoro Mjini hadi kijiji cha Mvuha (KM 78) Kwa lengo la kuunganisha Morogoro Mjini na kituo cha treni ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kilichopo eneo la Kisaki na hivyo kuongeza idadi ya wasafiri na shehena ya mizigo itakayotumia usafiri wa treni hiyo.

2

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (Mwenye Miwani), akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mngazi mkoani Morogoro, wakati alipokagua barabara ya Morogoro- Kisaki (KM 133) ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

 

“Tunatambua umuhimu wa barabara hii kwa wananchi wa Morogoro na mikoa ya jirani na sasa tunaendelea na mipango ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika hata vipindi vya masika”, amesisitiza Mhandisi Ngoyani.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutachochea fursa za utalii katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi na Mbuga za Selous kwa kuunganisha na mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya na hivyo kukuza pato la Taifa kupitia utalii.

Mhandisi Ngonyani ameeleza kuwa ujenzi huo utaanza kwa kujenga daraja jipya la Dutumi ambalo limekuwa halipitiki wakati wa masika pamoja na kukarabati Daraja la Mto Mvua ili liweze kuwa katika ubora unaostahili na kupitisha maji kwa urahisi bila kusababisha madhara kwa wakazi wa eneo hilo.

1

Mwenyekiti wa wa kijiji cha Mngazi, mkoani Morogoro akitoa maoni kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, wakati alipokagua barabara ya Morogoro- Kisaki (KM 133) ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Naye, Mhandisi Mkuu wa Mkoa kutoka Wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Godwin Andalwisye, amesema kuwa hatua za awali za ujenzi wa daraja la Dutumi umeanza ambapo usanifu wa kina umeshafanyika.

“Kwa sasa tumeshaandaa michoro itakatumika katika ujenzi wa daraja hili, tutahakikisha ujenzi wake unaanza na kukamilika kwa wakati ili kuimarisha sehemu hii na kupitika kwa urahisi hata wakati wa masika”, amesisitiza Mhandisi Andalwisye.

Katika hatua nyingine Mhandisi Ngonyani amemhimiza Mkandarasi wa GNMS anayejenga barabara ya Bigwa (KM 2) kukamilisha ujenzi wake kwa kiwango cha lami ifikapo Januari mwakani.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yupo Mkoani Morogoro katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Madaraja na Reli.

3

Muonekano wa Daraja la Ruvu lililopo katika barabara ya Morogoro –Kisaki (KM 133), ambapo barabara hiyo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. (Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).

Share:

Leave a reply