Benki ya Exim yaipiga tafu Hospitali ya Mwananyamala

97
0
Share:

Katika kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, Benki ya Exim Tanzania kupitia mradi wa“miaka 20 ya kujali jamii” imekabidhi vitanda na magodoro 40 kwa Hospitali ya rufaa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Matawi ya benki ya Exim, Agnes Kaganda alisema, “Katika kuadhimisha sherehe za wanawake mwezi huu, Benki ya Exim inatambua mchango wa wanawake katika kujenga jamii na kwenye ukuaji wa uchumi.

“Msingi wa mpango wetu huu wa mwaka mzima wa kujali jamii ni kuelewa kiasi gani wanawake ni muhimu katika jamii. Benki imejitolea kusherehekea maadhimisho ya miaka 20 kwa kusaidia wanawake kwa kuboresha huduma za uzazi katika sekta ya afya. Tunaamini kwamba tuna sehemu kubwa ya kufanya mabadiliko mazuri katika sekta mbalimbali katika jamii zetu na sisi tumejizatiti kwenye mpango huu.”

Nae Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, DkT. Khadija Shebe alipongeza Exim Bank Tanzania kwa msaada wake na kuhimiza taasisi mbalimbali kutekeleza ishara ya Benki ya Exim Tanzania katika kusaidia kuboresha huduma ya afya kwa wanawake nchini.

“Upungufu wa vitanda katika mahospitali ni changamoto kubwa. Msaada huu kutoka benki ya Exim wa hivi vitanda 40 na magodoro utasaidia sana katika kupunguza changamoto hii,” alisema Shebe.

Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam ni hospitali ya nane kupokea mchango huu, baada ya hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga mwezi uliopita, hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mbeya mwezi Januari, hospitali ya Mount Meru, Arusha mwezi Desemba, Hospital ya rufaa Dodoma mwezi Novemba, hospitali ya rufaa Ligula, Mtwara mwezi Oktoba, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Unguja, Zanzibar mwezi Septemba na Hospitali ya rufaa Temeke, Dar es Salaam mwezi wa nane mwaka jana.

Share:

Leave a reply