Bodi ya mfuko wa barabara yatakiwa kuzingatia thamani ya fedha; Prof. Mbarawa

307
0
Share:

Bodi ya Mfuko wa Barabara Nchini (RFB) imetakiwa kuhakikisha thamani ya fedha na ubora vinazingatiwa katika ujenzi wa miradi yote inayotekelezwa kwa kutumia fedha zinazotolewa na bodi hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa nne la ofisi ya Makao Makuu ya Bodi hiyo eneo la Njedengwa, Dodoma.

“Hakikisheni mnazingatia thamani ya fedha kwenye miradi yote inayotekelezwa kwa kutumia fedha za mfuko huu kwa sababu fedha hizo zinatokana na kodi za wananchi”, amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameipongeza Bodi hiyo kwa kumpatia kazi mkandarasi mzawa wa kampuni ya M/S Rans Company Ltd kutoka Zanzibar kujenga jengo hilo na pia kutumia Mhandisi Mshauri kutoka Serikalini ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).

“Nimefurahi kusikia TBA ndio msimamizi wa ujenzi wa jengo hili kwani naamini atasimamia ujenzi huu kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Makame Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Wenyeviti wa Bodi na Wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la ofisi za Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.

Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kufatilia na kufanya ukaguzi wa kina wa matumizi ya fedha za barabara zilizopelekwa katika Halmashauri ili kuangalia thamani ya fedha kama imezingatia viwango na ubora wa ujenzi wa miundombinu hiyo.

Pia amezitaka Bodi za Usajili wa Wakandarasi na Wahandisi kusimamia miradi inayotekelezwa ili kutimiza malengo ya kuwapa watanzania miundombinu bora itakayowafikisha kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Bw. Joseph Haule amesema ujenzi wa jengo la ofisi hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali kuhamishia ofisi zake mjini Dodoma.

James Wanyancha

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Dkt. James Wanyancha akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya bodi hiyo, Dodoma.

Aidha, ujenzi wa jengo hilo utapunguza gharama za shilingi milioni 420 kwa mwaka ambazo bodi inalipa katika jengo wanalokodi la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. James Wanyancha amefurahishwa na hatua hiyo ya ujenzi wa jengo kwani muda mrefu Serikali imekuwa na dhamira ya kuhamishia shughuli zake Dodoma ili kutimiza ndoto za Muasisi wa Taifa Hayati Mwl. Julius J. K Nyerere ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Serikali.

“Kutokana na dhamira hiyo ya Serikali bodi iliamua kujenga jengo la ofisi yake hapa Dodoma mwaka 2014 na leo tutapata fursa ya kuweka jiwe la msingi kuashiria kuanza ujenzi wake rasmi”, amesema Dkt. Wanyancha.

Ujenzi wa jengo hilo utagharimu takribani kiasi cha shilingi bilioni sita ambapo hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 72 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti mwaka huu.

Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Joseph Haule

Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi za bodi hiyo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa mkoani Dodoma.

Joseph Nyamhanga

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga (Kulia) akizungumza na Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule (Kushoto) kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa ofisi za bodi hiyo, mkoani Dodoma.

Profesa Makame Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto) akifunua pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi wa jengo la ofisi za Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), mkoani Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga, kushoto ni Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt. James Wanyancha.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Dkt. James Wanyancha (kushoto) mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa ofisi za bodi hiyo mkoani Dodoma.

Muonekano wa jengo la ofisi ya Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), linalojengwa eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.

Muonekano wa jengo la ofisi ya Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), linalojengwa eneo la Njedengwa mkoani Dodoma.

Makutupora

Kikundi cha Ngoma kutoka Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Makutupora kikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini(RFB), mkoani Dodoma.

Share:

Leave a reply