Chama cha Wakandarasi Tanzania waomba kupewa nafasi kuijenga Dodoma, wampongeza Rais Magufuli

881
0
Share:

Chama cha Wakandarasi Tanzania (CATA) kimepongeza juhudi  za utawala wa Rais Dk. John Magufuli  kwa kuendeleza ujenzi wa Taifa hususani wa Miundombinu na  Majengo mbalimbali nchini huku wakiunga mkono kauli yake ya hivi karibuni ya Serikali ya awamu ya tano na taasisi zake kuhamia Dodoma ambapo chama hicho kimesema uamuzi huo ni shauku kubwa na iwe kama changamoto kwa wakandarasi wa hapa nchini kushiriki katika uamuzi huo kikamilifu.

Wakizungumza mapema leo  17 Februari 2017, Jijini Dar es Salaam, uongozi wa chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, wamebainisha kuwa wanafikisha  ombi lao kwa Mheshimiwa Rais kuhusiana na tamko la hivi karibuni lililotolewa na Serikali kwa Wakala wa Majengo nchini (TBA)  na baadhi ya taasisi za Umma hapa nchini, kukabidhiwa uhimili wa kushughulikia  ujenzi wa miradi ya umma hasa majengo.

“Kwa vyovyote  vile tunatarajia msukumo mkubwa katika kutekeleza azma hiyo. Na hivyo basi matarajio ni wakandarasi wa hapa nchini kushirikishwa katika zabuni mbalimbali za miradi ya Umma.

Hivyo basi, ombi letu kwa Serikali ya awamu hii ya tano, ni kuwashirikisha katika zabuni zake wakandarasi woet wa Kitanzania, wakiwemo Wakandarasi wa madaraja yote ili waweze kujijenga kitaalam katika utekelezaji miradi na kuongeza ajira ya vijana katika makampuni hayo” ameeleza Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, Injinia Lawrence Mwakyambiki wakati wa mkutano huo kwa waandishi wa habari.

Aidha, Mwenyekiti huyo Taifa, amesisitiza kuwa, ombi la chama chao kwa Rais Magufuli  linazingatia maazimio yaliyopitishwa katika mikutano ya majadiliano kati ya Bodi ya Wakandarasi Tanzania na Wakanadarasi wenyewe iliyofanyika Mei 2016 ambapo waliazimia taasisi za Umma pamoja na Wizara kuwa na miradi ya kipekee wa lengo la kujenga uwezo wa Wakandarasi wa Kitanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakandarasi Tanzania kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia  John Bura amebainisha kuwa, Wakandarasi wa Tanzania wamekuwa katika mstari wa mbele katika kufanya kazi za kizalendo  hivyo wanapongeza juhudi za Rais Magufuli kwa kuwajali wakandarasi wa ndani.

“Tunashukru  Rais Magufuli na wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS kwa kuitikia wito wa Wakandarasi  kutengewa miradi michache ambayo ilikwisha tangazwa, Tunapongeza sana kwa hilo na salamu zetu zifike kwa Rais wetu” ameeleza Injia Bura.

Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania (CATA) pia kimewaomba wanachama wake kote nchini kujitokeza na kulipia malipo yao ya ada  yaliyo kisheria ili kufanikisha malengo ya chama hicho.

Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, Injinia Lawrence Mwakyambiki (kulia) akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa mkutano huo waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa Wakandarasi Tanzania kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia  John Bura akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani)

Share:

Leave a reply