CUF Lipumba yadaiwa kuendelea kuiuzia majimbo CCM

244
0
Share:

Baada ya Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza nia ya kushiriki katika uchaguzi mdogo wa marudio ili kutetea jimbo la Kinondoni, baada ya Mbunge wake Maulid Mtulia kujiudhuru na kujiunga na CCM.

CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sherrif Hamad umeibuka na kudai kuwa, CUF upande wa Lipumba wameliuza jimbo la Kinondoni kwa CCM ili iendelee kufanya biashara na chama hicho ya kuua upinzani nchini.

Madai hayo yalitolewa jana na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi upande wa Maalim Seif, Shaweji Mketo alipozungumza na mtandao huu kwa njia ya simu ambapo amedai kuwa, “Wao ndio waliouza jimbo sasa wametangaza kushiriki uchaguzi ili waendelee kufanya biashara na CCM. Sisi tutatoa utaratibu wetu muda si mrefu.”

Dewji Blog ilimtafuta Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi upande wa Prof. Lipumba, Jafari Mneke ili kupata ufafanuzi wa madai hayo kwa njia ya simu, ambapo amekanusha tuhuma hizo kwa madai kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuthibitisha madai hayo, na kwamba hizo ni porojo kutoka kwa watu waliofilisika kisiasa.

“Hizo ni porojo tu ambazo hazina mashiko kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kuthibitisha hilo, kwa hiyo siwezi kuzungumzia hizo porojo sababu zinatoka kwa watu waliofilisika kisiasa. Kwanza kuhusu Mtulia kutuunga mkono hakuna mwenye uwezo wa kuthibitisha hilo, yule ni mbunge ambaye muda wote waliungana na Maalim uthibitisho upo tangu mkutano mkuu uliovurugika na muda wote akishirikiana na Chadema, wabunge wetu walikuwa Naftaha Nachuma na Sakaya,” amesema.

Kuhusu tetesi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wabunge wa CUF kuendelea kung’oka na kujiunga na CCM, Mneke amedai kuwa, hakuna taarifa na au viashiria vinavyoonyesha kwamba kuna wabunge wengine wa chama hicho wanampango wa kujiuzulu.

“Kuhusu uchaguzi wa marudio tunajipanga kutetea jimbo, WanaKinondoni waliamini CUF na kuipa ridhaa kosa letu lilikuwa kumpa mtu asiye makini, tuna simama kama chama kuhakikisha tunatetea jimbo libaki CUF. Tutatangaza mgombea hivi karibuni,  wanachama wengi tutamchagua mwanachama makini atakayeshika nafasi hiyo,” amesema Mneke.  

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply