Dar yaongoza kwa ajali za barabarani

558
0
Share:

Serikali imesema kuwa Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa  kuwa na ajali nyingi za barabarani kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 zilizosababisha vifo vya watu pamoja na majeruhi.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Rwegasira  kuhusu kuongezeka kwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mhe. Masauni kwenye taarifa hiyo Jiji la Dar es Salaam limeongoza kwa kuwa na ajali 18,506 kati ya ajali 46,539 zilizotokea nchi nzima kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015.

“Takwimu za nchi nzima zinaonesha kuwa Mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo 4,002 na majeruhi  20,689. Mwaka 2014 zilitokea ajali 14,360 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015 zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383,” alisema Masauni. 

Mhe. Masauni alieleza kuwa kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kipolisi Kinondoni uliongoza kwa kuwa na ajali zipatazo 6,589 ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Ilala uliokuwa na ajali 3,464 wakati Mkoa wa Simiyu na Tanga kulikuwa na ajali chache ambapo Simiyu zilitokea ajali 67 na Tanga ajali 96. 

Mwaka 2014 Kinondoni na Ilala ziliongoza tena kwa kuwa na ajali 3,086 zilizotokea  Kinondoni na Ilala ajali 2,516 na mikoa iliyokuwa na ajali chache ni Simiyu ajali 55 na Kagera ajali 29.

Aidha, Mhe. Masauni alisema kuwa mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi Ilala uliongoza kwa kuwa na ajali nyingi za barabarani ambapo ajali 2,516 zilitokea mkoani humo ikifuatiwa na Temeke uliokuwa na ajali 1,420 wakati mikoa ya Rukwa na Arusha ilikuwa na ajali chache. 

Mhe. Masauni alibainisha kuwa mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu  hizo ni kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Polisi Annual Report) ambapo kila mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.

Na Fatma Salum – MAELEZO, Dodoma

Share:

Leave a reply