DC Hapi apiga marufuku wenyeviti kuchangisha michango wananchi bila ya idhini ya Manispaa

475
0
Share:

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amewapiga marufuku viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata kuchangisha wananchi fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo bila ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Aaron Kagurumjuli.

Hapi ametoa maagizo hayo leo katika ziara yake ya mwisho kwenye Kata ya Makongo Juu baada ya kubaini ubadhirifu wa fedha za wananchi unaofanywa na baadhi ya viongozi wasio kuwa waaminifu.

Amesema uchangishwaji fedha za wananchi holela pasipo ridhaa ya manispaa ndiyo chanzo cha baadhi ya kata kushindwa kutoa taarifa sahihi za mapato na matumizi.

“Muepuke kujichangishia fedha kwa wananchi bila kupata kibali kutoka kwa mkurugenzi. Tabia ya kuchangisha fedha kinyume cha taratibu ndiyo chanzo cha malalamiko, rushwa na ubadhirifu wa fedha za wananchi na kusababisha miradi husika kushindwa kutekelezwa,” amesema na kuongeza.

“Kama wananchi wanataka kuchanga fedha wapewe utaratibu, wasomewe taarifa za mapato na matumizi, na kila anayechangishwa fedha apewe risiti za machine za kielektroniki.”

Sambamba na hilo, Hapi ameendelea kuwasisitiza wakuu wa shule kutowachangisha wanafunzi fedha na kwamba shule itakayobainika kuchangisha fedha wanafunzi, mkuu wa shule atachukuliwa hatua.

“Serikali imepiga marufuku shule zote kuchangisha wanafunzi fedha za michango inayohusisha wanafunzi na waalimu, wazazi kama mnataka kuchangia mfanye wenyewe pasipo kushirikisha mwalimu au mwanafunzi,” amesema.

Share:

Leave a reply