DC Ikungi ahimiza ufayaji wa mazoezi kuepuka magonjwa

438
0
Share:

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu ameshiriki kufanya mazoezi ya viungo na  wananchi  wa Kata ya Makiungu na Mungaa zilizopo wilayani humo huku akitilia mkazo ufanyaji wa mazoezi hayo sambamba na uzingatiaji wa  ulaji wa vyakula visivyo na mafuta mengi ili kuepukana na maradhi yasiyoambukiza.

Hatua hiyo ni kuunga mkono maelekezo ya makamu wa Rais Samiah Suluhu Hassan ya kufanya mazoezi kila jumamosi ya pili ya kila mwezi.

Akizungumza katika mazoezi hayo Mtaturu amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakichukua maisha ya watu wengi duniani hivyo ni wakati wa kuweka jitihada kupambana  nayo.

“Mbali na kufanya mazoezi haya kila mwezi lakini ni vizuri pia kuweka utaratibu wa kutembea walau mara moja kwa siku iwe asubuhi au jioni lakini pia kuweka msisitizo kwenye ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi huku tukiepuka matumizi ya mafuta mengi kwenye vyakula vyetu,”alisema Mtaturu.

Alisema rais John Magufuli anasisitiza kauli mbiu yake ya hapa kazi tu na ili kauli mbiu hiyo iweze kufanikiwa ni lazima tuwe na afya iliyo imara kwa kujenga tabia ya kupima mara kwa mara na kufanya mazoezi.

“Ili kuweka mazoea ya ufanyaji wa mazoezi tunapaswa tuanze kuwazoesha vijana wadogo na ili kutilia mkazo hili hivi karibuni tutaanzisha ligi ya mpira wa miguu itakayoitwa Elimu Cup ambayo  itakashirikisha kata zote 28 wilayani hapa,”aliongeza mkuu huyo.

Aliweka bayana lengo la kuanzisha ligi hiyo kuwa ni  kuhamasisha uchangiaji wa mfuko wa elimu na hapo hapo kubaini vipaji vya vijana.

Kauli mbiu ya kuhamasisha mazoezi hayo ni mazoezi ni  afya tokomeza magonjwa  yasiyoambukizwa.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu  akizungumza na wananchi wa kata ya Makiungu na Mungaa  kwenye viwanja vya Mission Makiungu baada ya kumaliza kufanya mazoezi ya viungo.

Share:

Leave a reply