DC Manyoni awatia mbaroni watu watatu kwa kuruhusu ndugu yao kuoa mwanafunzi

398
0
Share:

Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Geoffrey Mwambe amefanikiwa kuzuia msichana mwenye umri wa miaka 14 (jina tunalo) kuolewa na ameagiza arejeshwe mara moja shuleni kuendelea na masomo yake.

Mtoto huyo aliachishwa shule mwaka juzi 2015 akiwa darasa la sita katika shule ya msingi Idodiandole halmashauri ya Itigi wilaya ya Manyoni.

Imeelezwa kwamba mtoto huyo aliachishwa shule kutokana na tatizo la ugonjwa wa kifafa lakini miezi mitatu baada ya kuachishwa shule, mchakato wa kuozeshwa ulianza kufanyika. 

“Fundi mwashi Jeremieah Antony (20) mkazi wa Mwanzi Manyoni mjini aliweza kumuoa mwanafunzi huyo kwa ndoa ya kimila nyumbani kwa mama mzazi wa bwana harusi,” alisema Mwambe.

Mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa wazazi wa binti huyo walitumia kigezo cha ugonjwa wa binti yao, kumwachisha shule na kufanya juhudi za kumwozesha, ili waweze kujiepusha na shida ya kumuhudumia.

Mwambe alitumia nafasi hiyo kukemea vikali vitendo vya kuoza wasichana wadogo hasa wanafunzi na kwamba watakaokamatwa kwa tuhuma hizo, watachukuliwa hatua kali za kisheria.

 Aidha, alisema bwana harusi Jeremiah, mama wa bwana harusi Janeth Makole na kaka wa bwana harusi Alexander Anthony, wamefikishwa polisi kwa uchunguzi zaidi wakati wazazi wa mwanafunzi huyo, bwana na bibi Robert Mlewa wanaendelea kutafutwa.

Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya, amemwagiza  Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Manyoni, amlipie gharama za sare na vifaa vya shule na afisa elimu na ofisa maendeleo ya jamii wamsimamie na wawe walezi wake kuhakikisha anafika mbali kielimu.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wenyeviti wa vitongoji vya Samaria na Mwanzi, mtendaji kata na diwani kata ya Manyoni, kwa kunipatia taarifa hii iliyofanikisha kuzuia ndoa hii haramu,” alisema.

Kwa upande wake mwanafunzi huyo, amesema hapo awali aligoma kuolewa, lakini kutokana na shinikizo la wazazi wakidai tayari wamekula mahari na hawana uwezo wa kurejesha, hivyo hakuna namna lazima aolewe, ndipo kukubali kwa shingo upande kutii amri ya wazazi.

Na Nathaniel Limu, Manyoni

Share:

Leave a reply