Familia: Taasisi ya kwanza ya malezi ya watoto

377
0
Share:

Familia ni kundi la watu kijamii linalofanana watu waliozaliwa damu moja, kuishi pamoja au kuoana. Familia huundwa na Mume, Mke, Watoto, Ndugu kama wajomba, kaka, shangazi, baba mdogo, babu, bibi nk. Watoto ni zao la familia. Watoto ni kiungo muhimu cha familia. Watoto wanapozaliwa, ukuaji wao huanzia katika familia. Zipo Taasisi nyingi ambapo zina mchango katika malezi bora ya watoto, lakini familia ni taasisi yenye nguvu kubwa sana katika kuamua aina ya tabia ya mtoto.

Katika Makala hii nitachambua nafasi ya familia katika malezi ya watoto. Familia ni taasisi ya kwanza kabisa katika suala la malezi ya watoto katika jamii. Kama wazazi watatimiza wajibu wao huu muhimu wa malezi, mtoto atakuwa katika malezi bora na kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii. Wazazi, Walezi na  Ndugu wengine wana wajibu mkubwa wa kutoa malezi bora kwa mtoto. Hata Maandiko Matakatifu ya Biblia yanasema “Mlee Mtoto Katika Njia Impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (Mithali 22:6). Mtoto ana imani kubwa kutoka kwa wazazi, walezi na ndugu zake wanaomzunguka.

Katika hatua za malezi, ubongo wa mtoto huwa hauna mambo mengi. Na huu ndo muda muafaka wa wanafamilia kupandikiza mbegu ya malezi bora kwa watoto kabla mtoto hajakumbana na  mambo mengine ya kidunia yanayoweza kupata nafasi katika ubongo wake. Malezi ya familia yana nafasi kubwa katika kujenga mambo mazuri kwa mtoto kama vile:

Mosi, Kuwa na heshima na nidhamu nzuri. Kama nilivyotangulia kusema familia ndio msingi wa mambo mazuri kwa mtoto. Suala la heshima na nidhamu linaeleweka vizuri kwa mtoto kama wanafamilia watamfundisha katika hatua za awali za maisha yake. Jamii itakuwa na raia wengi wenye heshima na nidhamu. Waswahili wanasema “ Samaki Mkunje Angali Mbichi”.

Mbili, Kupenda elimu. Kabla mtoto hajapata msisitizo wa kupenda elimu kutoka kwa mwalimu wake shuleni, msisitizo huo anapaswa kuupata kutoka nyumbani kwenye familia anayotoka. Walimu wanapata kazi ngumu ya kuwaelekeza wanafunzi umuhimu wa elimu kwa sababu mtoto anashindwa kuona umuhimu huo kwa sababu watu wake wa karibu wa familia hawamwelezi umuhimu wa elimu. Kuna kisa kimoja niliwahi kukisikia ambacho kilimtoke mwalimu mmoja ambaye alijibiwa vibaya na mwanafunzi baada ya mwalimu kumsisitiza mwanafunzi umuhimu wa elimu na kusoma. Baada ya Mwalimu kuongea na mwanafunzi kuhusu umuhimu wa elimu, mwanaunzi alimjibu Mwalimu kwa dharau kwa kusema “ Mwalimu acha kufuatilia maisha yangu, baba mwenyewe haniambii nisome, wewe ni nani mpaka uniambie?”. Je ingekuaje kama mtoto huyu angepata msisitizo wa kusoma kutoka kwa wazazi au wanafamilia wake? Nadhani asingethubutu kumjibu mwalimu wake maneno hayo. Familia zikisimama kwenye nafasi zao, basi tutawapunguzia kazi walimu wetu kwa mambo ambayo yalipaswa kuanzia kwenye familia. Mwalimu ni mtu wa kusisitiza kile ambacho wanafamilia wameanza nacho nyumbani, lakini kumfanya mwalimu kuwa msemaji mkuu na wa kwanza ni makosa makubwa sana na somo linakuwa gumu kueleweka kwa mtoto.

Tatu, Kupenda na kuyatii mafundisho ya dini. Ili kujenga jamii yenye raia wanaotii mafundisho ya dini, ni muhimu sana familia ikawapa watoto malezi bora ya dini wakiwa watoto wadogo. Ili Viongozi wa dini waeleweke kwa urahisi wawapo makanisani na misikitini, mafundisho ya dini hupaswa kuanzia nyumbani. Mwimbaji mmoja wa nyimbo za Injili aliimba wimbo uitwao “ Ibada njema huanzia nyumbani”. Mtoto aliyelelewa katika kupenda mafundisho ya dini huwa mtoto mwenye tabia nzuri ambazo wanajamii hufurahishwa nazo.

Nne, Kupenda kufanya na kusaidia kazi za nyumbani. Msingi wa mtoto kupenda kushiriki kazi za nyumbani unajengwa katika familia. Baadhi ya wazazi huwadekeza watoto na kufikia hatua mtoto anakatazwa kufanya kazi ndogondogo kama kufua nguo zake, kutandika kitanda chake, kuosha vyombo. Kazi hizi huachiwa dada wa kazi, huku mtoto akitumia muda huo kuangalia runinga. Hii ina athari mbaya sana hasa pale mtoto anapofikia umri wa kujitegemea, anajikuta hajui kupika, kufua nk. Taasisi ya familia ina jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto analelewa katika mazingira ya kupenda kufanya kazi na kusaidia kazi za nyumbani kwa faida yake mwenyewe hapo baadae.

Tano, Kujiepusha na marafiki wasio na tabia njema. Familia pia ina wajibu wa kuhakikisha inatoa mwelekeo na mwongozo mzuri kwa mtoto kuhusiana na aina za marafiki ambao mtoto wao anapaswa kuwa nao. Marafiki wana ushawishi mkubwa sana katika kumfanya mtoto awe na tabia nzuri au tabia mbaya. Ni muhimu sana kwa wanafamilia kumuelimisha mtoto wao kuambatana na marafiki ambao wataleta matokeo chanya katika maisha yake. Mfano kuwa na marafiki wanaopenda elimu, wenye nidhamu bora, wenye utii, wanaopenda kusaidia wazazi kazi za nyumbani.

Kwahiyo, wanafamilia wana wajibu mkubwa katika malezi ya mtoto ili kumjenga mtoto kuwa na tabia njema na mwelekeo mzuri wa maisha. Kama watoto watapata malezi bora katika familia zao, basi tutajenga jamii yenye raia wema na wawajibikaji kwa maisha yao, jamii na nchi yao. Uwekezaji wa malezi bora ufanywe katika umri mdogo na uanzie katika familia. Tafakari.

Katika Makala ijayo nitajadili taasisi nyingine zenye mchango  wa malezi bora kwa watoto.

Mwandishi wa Makala hii Reubeni Lumbagalani Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0764-666349.

Share:

Leave a reply