Guardiola afurahia sare ya Man City na Liverpool

696
0
Share:

Licha ya timu yake ya Manchester City kutoa sare ya goli 1-1 na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema matokeo hayo yamemfurahisha sana.

Guardiola alisema alipenda jinsi wachezaji wake walivyocheza dhidi ya Livepool lakini anawalaumu kwa kushindwa kupata alama tatu ambazo zingewafanya wapande juu zaidi katika msimamo wa EPL.

“Huwezi kuamini, hii ni moja ya siku ambayo nina furaha sana katika maisha yangu nikiwa kama kocha. Baada ya kupoteza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa siku mbili tulikuwa na huzuni katika mazoezi na hata hatukuwa tukizungumza sana,” alisema Guardiola na kuongeza.

“Tuliwasili uwanjani katika mchezo wa Liverpool tukifahamu fika hawana mchezo wowote wa Ligi ya Ulaya kwa mwaka mzima na hivyo walikuwa na wiki nzima ya kujiandaa kwa mchezo wetu, na kwa jinsi tulivyopambana na kukimbia na tulivyokuwa na muunganiko baina yetu, ilikuwa ni siku nzuri sana kwangu.”

Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Etihad, Liverpool walikuwa wa kwanza kupata goli kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 51 kupitia kwa James Milner na katika dakika ya 69 Sergio Aguero aliisawazishia Man City na hadi mchezo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana goli 1-1.

Share:

Leave a reply