Halotel kutumia Bilioni 200 kuboresha huduma za mawasiliano

780
0
Share:

Zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 200 za Kitanzania zimewekezwa na Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Halotel, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maboresho ya huduma za mawasiliano nchini Tanzania hususani huduma za intaneti na mawasiliano ya simu kwa mwaka 2017,

Uwekezaji huu unaifanya kampuni hiyo kuwa kampuni ya kwanza kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha huduma za mawasiliano Tanzania. Katika kipindi cha hivi karibuni kufuatia uwekezaji huo mkubwa ilioufanya, imefanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano kwa zaidi ya asilimia 95% ya Watanzania nchi nzima.

Akizungumzia juu ya uwekezaji huo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Halotel Tanzania, Bw. Lee Van Dai, amesema kuwa maboresho hayo yanalenga kuboresha huduma za mawasiliano hususani kuongeza ubora na kasi ya intaneti kwa wateja wa mtandao huo pamoja na kushusha gharama kwa kiasi kikubwa.

“Katika kuendelea kutekeleza jitihada za serikali katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini, kampuni yetu imepanga kutumia zaidi ya bilioni 200 za Kitanzania. Fedha hizo zitatumika ili kuboresha huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma bora miongoni mwa Watanzania. Sisi tumeendelea kuwa kampuni ya kwanza ya simu kuendelea kuthubutu kuwekeza katika huduma za mawasiliano kwa kiasi hicho kikubwa ili kutoa huduma za uhakika.” alisema Dai.

Aidha alibainisha kuwa, uwekezaji huo ni sehemu ya kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali kuhitaji kampuni kubwa kuendelea kuwekeza nchini na kuboresha huduma kwa jamii ya Watanzania, hivyo uwekezaji huu unaendana sambamba na kupunguza gharama za mawasiliano hususani za vifurushi vya intaneti kwa wateja wetu.

“Tumesikia kilio cha Watanzania ambao wameendelea kulalamikia gharama za mawasiliano kuendelea kupanda siku hadi siku na ubora wa huduma ukiwa mdogo kitu ambacho kinaathiri matumizi yao. Maboresho haya yanalenga kuwapatia kwanza, intaneti yenye ubora zaidi na vifurushi zaidi kwa kiasi kidogo cha fedha ambacho kinaendana na mahitaji ya kila mteja.” alisema Dai.

“Tunatambua teknolojia ya mawasiliano imekua kwa kiasi kikubwa na inatumika katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Sekta hii imekuwa ni kiungo kizuri katika upashanaji wa habari hususani mitandao ya kijamii ambayo ndio njia rahisi na ya haraka kuwafikia watu. Hivyo basi, maboresho haya yanalenga kuendelea kuwapatia Watanzania muda zaidi wa kuendelea kuungana na jamii kwa kufurahia vifurushi vikubwa kwa kiasi kidogo cha fedha.” aliongezea Mkurugenzi huyo.

Ameendelea kufafanua kuwa “Hadi sasa Halotel tumeweza kuvifikia vijiji zaidi ya 3000 nchi nzima ambapo kitakwimu ni sawa na kuweza kufikia Tanzania kwa asilimia 95% hadi hivi sasa. Pia tumeunganisha mtandao wetu kwa zaidi ya Kilomita 20,000 za mkongo wa mawasiliano. Hii inafanya huduma zetu kuwa ni za uhakika na kutufanya kinara katika kuyafikia maeneo mengi zaidi kuliko mtandao wowote nchini.”

Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha cha Bidhaa na huduma wa Halotel, Deogratius Shio amesema kuwa licha ya uwekezaji ambao kampuni yake inafanya wao kama kitengo cha bidhaa wamefanya maboresho ya vifurushi vyao yatakayo endana sambamba na uwekezaji huo.

“Licha ya uwekezaji tunaofanya kwa hali ilivyo ngumu sasa miongoni mwa Watanzania tumeboresha zaidi vifurushi vyetu ambapo sasa kwa Shilingi 499, mteja atapata MB 200. Kiwango hiko ni kikubwa zaidi cha MB kinachotolewa ukilinganisha ni mitandao mingine kwa zaidi ya 100%. Kwa Shilingi 1000, mteja anaweza kupata MB 450, pamoja na vifurushi vingine vingi. Hivyo nawasihi Watanzania kuendelea kujiunga na Halotel ili waendelee kufurahia huduma zetu kwa gharama nafuu.” alisema Shio

Kampuni ya Halotel licha ya kuwekeza zaidi katika mfumo wa mawasiliano ya simu pia inatoa huduma kwa gharama nafuu zaidi kwa mamilioni ya Watanzania. Dhumuni kuu ni kuwapunguzia gharama na kuwawezesha kuendelea kufurahia huduma za intaneti zenye uhakika zaidi.

Share:

Leave a reply