Heche amshukia DC Luoga, amtuhumu kusaini mkataba wa kifisadi wa uwekezaji

919
0
Share:

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, John Heche amemshukia na kumtuhumu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga kuwa amesaini mkataba wa uwekezaji kinyume cha sheria sambamba na kutumia nguvu na vitisho kwa wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kupora ardhi yenye hekta zaidi ya 34,000 linalokaliwa na wakazi zaidi ya 30,000, kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha miwa.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari, Aprili 12,2017 jijini Dar es Salaam, Heche amedai kuwa, Luoga alisaini mkataba huo kwa kutumia muhtasari feki wa kijiji,  pasipo kuwepo uwazi, ushirikishwaji wa wananchi pamoja na chombo chao cha uwakilishi yaani baraza la madiwani.

Aidha, ameeleza kuwa tangu mwezi Januari, 2017 wananchi wa Jimbo lake walimpatia taarifa za uwekezaji huo, na kwamba alizungumza na Luoga, ambaye alimhakikishia kuwa hakuna ardhi ya mwananchi itakayochukuliwa pasina kulipwa fidia, ndipo alipomtaka DC huyo kabla ya kusaini mkataba ahakikishe uwepo wa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi ili kujadili faida na hasara ya mradi huo, lakini Luoga hakuyafanya hayo.

“Kuonesha kuwa mradi huu hauna uhalali, serikali ya wilaya kupitia Mkuu huyo wa wilaya baada ya kukiuka taratibu zote zinazotakiwa kutwaa ardhi ya wananchi wameanza kukamata kutisha kubambikizia watu kesi hata kulaghai ili kulazimisha uwekezaji,” amesema na kuongeza.

“DC hawezi kujadili mkataba kwa ajili ya wananchi, kaita wazee wa mila na maarufu pasipo kuita baraza la madiwani lenye madiwani zaidi ya 32 wanaowakilisha wananchi. Hili tutalipambani sababu sheria haziruhusu kumilikisha ardhi raia wa kigeni, nasikia huyo muwekezaji anatoka Uganda na anatumia madalali kupata ardhi hiyo.Inawezekana wamegundua madini katika eneo hilo na kwamba wanatumia mgongo wa kilimo cha miwa ili baadae akishapata eneo hilo kila kilichopo pale kiwe ni chake,”

Amesisitiza kuwa, mkataba huo unakiuka sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kifungu 3 inayosema lazima uwepo uwazi katika mradi pamoja na ushirikishwaji wa wananchi ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu manufaa kwa jamii nzima kutokana na uwekezaji huo.

“Kama hataleta huo mkataba kwa wananchi au kutolipwa fidia, namuandikia barua Waziri Mkuu au Waziri wa Ardhi kuingilia kati suala hili wasipochukua hatua tutapambana na mimi nitaongoza mapambano kulinda ardhi yetu,” amesema.

Amesema kuwa”Hatupingi uwekezaji au kiwanda kujengwa ila hatutakubali kitendo cha wananchi kutoshirikishwa  na kuuziwa ng’ombe kwenye gunia. Namtahadharisha DC asiturudishe katika matatizo mengine watu wa Tarime tumechoka kuumizwa kwa sababu ya uwekezaji,”

Katika hatua nyingine, amemtaka kutowachafua wananchi wa Tarime kwamba maeneo yao walikuwa wanalima bangi na kudai kuwa lengo lake ni kupotosha ukweli kwa kuwachafua ili kufanikisha lengo lake.

Hata hivyo, kufuatia tuhuma hizo, Modewjiblog.com ilimtafuta Luoga kwa njia ya simu kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo, ambapo amesema kuwa tuhuma hizo si za kweli.

“Hizo taarifa siyo za kweli sababu huo mkataba anaouzungumzia aliyeusaini ni mwenyekiti wa Halmashauri ambaye pia ni mwanachama wa chama chake hicho hicho, yaani siyo za kweli ila yeye anajisikia kusema ivyo,” amesema Luoga.

Na Regina Mkonde.

 

 

Share:

Leave a reply