Wafanyabiashara wamkumbusha Rais Magufuli ahadi alizowapatia

342
0
Share:

Baadhi  ya wakulima na wafanyabiashara wa vitunguu mkoani Singida, wameiomba serikali ya awamu ya tano kutekeleza ahadi  yake ya kufuta ushuru wenye manyanyaso na usio na tija kwa jamii.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wamedai kizuizi  cha mazao cha Iguguno wilaya ya Mkalama, Kijiji cha Kinyeto wilaya ya Singida, vimekithiri kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wakulima na wafanyabiashara wa zao la vitunguu.

Wamedai kwamba wakifika katika vizuizi, hupoteza zaidi ya saa tano wakivutana juu ya kiasi kikubwa cha ushuru kinachotozwa.

“Sisi wakulima tukishavuna vitunguu vyetu shambani, hatuweki  kwenye magunia huwa  tunavimwaga tu kwenye fuso au malori ya aina mbalimbali. Tukifika kwenye vizuizi watoza ushuru, wanakadiria kuwa tumesafirisha idadi kubwa ya magunia lengo lao likiwa ni kutoza ushuru mkubwa,” wamedai.

Mkulima wa vitunguu jimbo la Singida Kaskazini, Meshaki Munungudi, alisema wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana, wagombea mbalimbali wakiwemo wa nafasi ya Urais walikuwa wakiahidi kwamba, endapo watachaguliwa watafuta ushuru  ambao ni kandamizi.

Alisema anashangaa serikali hii, kabla na baada wakati wote wa kilimo haitoi msaada wowote kwa wakulima, lakini mkulima akivuna tu mazao yake, anakaliwa kooni kwa kutozwa ushuru.

“Serikali hii haimwekei mazingira mazuri mkulima na mfanya biashara, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na  kurejesha gharama zote za kilimo na kujipatia faida kwa maendeleo yake,”alisema Manugudi.

Akifafabua, alisema barabara na madaraja mengi yameheribiwa na mvua kubwa za mwaka huu, hazijafanyiwa matengenezo, na hivyo kuwa kero kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara.

Kwa upande wake mkulima na mfanyabiashara wa vitunguu, Japheti Kikong’oto, alisema Setikali iangalie upya suala la ushuru wa mazao, kwa madai kwamba ushuru unaotozwa hivi sasa, unachangia mkulima au mfanyabiashara akose faida kwenye shughuli zake.

“Manispaa ya Singida, imeacha wajibu wake kwenye soko la vitunguu Misuna imejikita tu kukusanya ushuru. Dampo la takataka lililopo hapa, limefurika takataka na wakati huu wa mvua, linaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko wakati wowote,” alisema Kinkong’oto

Naye Mwenyekiti wa soko la vitunguu Misuna mjini hapa, Joseph Mdoo, alisema soko hilo linaloiingiza  mapato makubwa Manispaa ila halina hata taa kitendo kinachosababisha ulinzi wa vitunguu na mali zingine kuwa ngumu mno nyakati za usiku.

“Manispaa yetu haijalipa hadhi soko letu, soko lina hadi makaburi ndani yake na vifusi vikumbwa vya udongo, mbaya zaidi soko lipo wazi halina fensi ya kuzuia watu kuingia kiholela,” alisema Madoo.

Mwenyekiti huyo alitaja changamoto nyingine kuwa soko hilo ambalo wakati wa msimu wa vitunguu huajiri mamia ya wakazi wa mkoa huu,halina choo cha kukidhi mahitaji.

Na Nathaniel Limu, Singida

IMG_4354

Baadhi ya akina mama na watu wengine wakichambua vitunguu na kuviweka kwenye gredi tayari kuuzwa kwa wanunuzi.Awali msimu ulipoanza,gunia moja lilikuwa likiuzwa kwa shilingi 180,000,jana bei ilikuwa imeteremka na gunia liliuzwa kati ya shilingi 80,000 na 120,000.

IMG_4357

Mwenyekiti wa soko la vitunguu la Misuna mjini hapa,Joseph Mandoo,akionyesha lundo la taka ngumu katika dampo la soko la vitunguu, ambazo hazijazolewa kwa muda mrefu na kutishia kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko.

IMG_4365

Kijana akishusha vitunguu kutoka kwenye lori ambavyo wakulima wamevileta katika soko la vitunguu Misuna mjini hapa,kwa ajili ya kuviuza.Usafirishaji wa kumwaga vitunguu kwenye gari bila kutumia magunia kama ilivyozoeleka,kunasababisha mvutano mkali kati ya wakulima na watu wanaokusanya mazao kwenye vizuizi.Kila upande ukikisia idadi ya magunia kwenye lori husika.  (Picha na Nathaniel Limu)

IMG_4371

Share:

Leave a reply