Hospitali zatakiwa kuwalinda wapokea kumbukumbu na maambukizi

174
0
Share:

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu ameziagiza hospitali mbalimbali nchini kuhakikisha zinachukua tahadhari za kuwalinda wafanyakazi wake kitengo cha kumbukumbu katika mazingira ya kupata maambukizi hasa wanapokuwa kazini wakitimiza majukumu yao.

Waziri, Mwalimu ametoa maagizo hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya kutoka wizara hiyo, Dk. Mohamed A. Mohamed alipomwakilisha katika hafla ya kufungwa kwa mkutano wa Chama cha Maofisa Kumbukumbu na Taarifa za Afya Tanzania (THERIA) zilizofanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mohamed alisema wizara hiyo, inatambua mazingira hatarishi ambayo wafanyakazi wa kitengo cha kumbukumbu wamekuwa wakifanyia kazi hasa ukizingatia wao ndio watu wa kwanza kukutana na wagonjwa kabla ya kufika kwa madaktari jambo ambalo linaweza kuzua maambukizi kwa magonjwa yaambukizwao kwa njia ya hewa.

“..Natambua pia mazingira mnayofanyia kazi wengi wenu yanayowafanya kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kwani nyie ndo wa kwanza kabisa kukutana na mgonjwa, kabla ya kuonana na daktari au mtaalamu wa vipimo, hivyo kupata maambukizi ya magonjwa hatarishi hasa yaambukizayo kwa njia ya hewa na mengineyo ni rahisi. Woizara yangu inapenda kuwaagiza Wakuu wote wa hospitali nchini kuhakikisha wanarekebisha mazingira mnayofanyia kazi ili kuondoa hali hii,” alisema Dk. Mohamed akimwakilisha waziri wake.

Aidha wizara hiyo pia iliahidi kushughulikia kero ya uhaba na ukosefu wa wafanyakazi wa taaluma ya utunzaji kumbukumbu za afya kwenye vituo vya afya na hospitali hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuzitaka hospitali na vituo hivyo kuajiri watu wenye taaluma halisi ya utunzaji kumbukumbu na kuhakikisha kada hiyo inapata muundo, stahili zake na kutambulika kama ilivyo kwa makundi ya kada nyingine.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Maofisa Kumbukumbu na Taarifa za Afya Tanzania, Rehema Mwaipaja akizungumza katika mkutano huo alisema kuwa THERIA ina umuhimu mkubwa hasa ukizingatia kuwa takwimu sahihi za afya ndio msingi bora kwa huduma kamilifu kwa jamii. Aliongeza kuwa uboreshaji wa hali ya ukusanyaji, uchambuzi na utunzaji wa takwimu sahihi za afya unachangia kuboresha tafiti mbalimbali za afya ambazo ni matunda ya ukuaji na uboreshaji wa huduma kiujumla.

“Nidhahiri kuwa ukuaji wa taaluma ya afya hutegemea sana tafiti mbalimbali zitokanazo na taarifa zilizokusanywa na kutunzwa kikamilifu kazi ambayo ni ya msingi kwa afisa kumbukumbu wa afya mahali popote anapofanya kazi, hayo yote huleta faida kwa wagonjwa, taasisi na kwa wafanyakazi,” alisema Bi. Mwaipaja.

Wanachama wa THERIA kutoka mikoa mbalimbali walikutana kwa siku mbili mfululizo katika wao mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine mkutano huo ulifanya uchaguzi kupata viongozi wapya wa chama hicho.

Mkurugenzi wa Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mohamed A. Mohamed (kulia) aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Bi. Ummy Mwalimu, akizungumza na wanachama wa THERIA kabla ya kufunga mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Maofisa Kumbukumbu na Taarifa za Afya Tanzania (THERIA), Rehema Mwaipaja akizungumza na wanachama wa THERIA kabla ya kufungwa kwa Mkutano wao juzi.

 

Katibu Mkuu wa Chama cha Maofisa Kumbukumbu na Taarifa za Afya Tanzania (THERIA), Rehema Mwaipaja akizungumza na wanachama wa THERIA kabla ya kufungwa kwa Mkutano wao juzi.

 

Share:

Leave a reply