IGP Sirro Kuwa mgeni rasmi siku ya Amani Duniani, kufanyika kesho Temeke

299
0
Share:

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Simon Sirro anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani katika uwanja wa Mwembe Yanga wilayani Temeke kesho Jumamosi (Septemba 22) asubuhi.

Maashimisho hayo ya mwaka huu yatalenga kuelimisha vijana kuhusu changamoto za uhamiaji pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza Amani kwa ajili ya maendeleo.

Kauli mbiu ya Mwaka huu ni, “Pamoja Katika Kudumisha Amani, Heshima, Usalama na Utu kwa wote”.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha UN jijini Dar es Salaam ameelezea kwamba Siku hii iliasisiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mwaka 1981 ili kusitisha mapigano katika nchi ambazo kuna vita lakini pia ili kuikumbusha jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza Amani.

Afisa huyo alisema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika hotuba yake hivi karibuni kwamba, “hali ya Amani duniani imevunjika vunjika vipande-kuna haja ya kurejea na kuwa kipande kimoja.” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesikitishwa na kuongezeka kwa vifo vinavyosababishwa na uvunjifu wa Amani duniani kote

“Tumewaalika vijana wajasiriamali na wasanii wachekeshaji ili watoe mfano kwa vijana wenzao kwamba inawezekana kubaki Tanzania na kuishi vizuri bila kuwazia kuzamia katika nchi za ugenini. Kila mmoja wetu ana jukumu la kulinda Amani, tunapaswa kutunza Amani na kuishi kwa namna ambayo haitahatarisha maisha.  Amani ikitoweka kila shughuli itasimama-hutaweza kuchat wala kutembea kutoka mahala pamoja kwenda kwingine kama ulivyozoea-kila sekta itaathirika.” Alisema Bi Stella.

Siku hii inaadhimishwa kila mwaka kwa ushirikiano wa wadau wa Amani wakiwemo Mashirika ya Jane Goodall’s-Roots and Shoots, Mtandao wa Dini kwa ajili ya Watoto(GNRC), Muungano wa Mashirika ya dini (IRCPT), Global Peace Foundation,Tanzania Bora Initiative, Chama cha Maskauti Tanzania, Voluntary Service Overseas (VSO), Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wahamiaji, Restless International na vijana waliopo nje ya shule.

 

Share:

Leave a reply