JPM ataka taarifa ya faida ya mabasi yaendayo kasi tangu yalipoanza kutoa huduma

639
0
Share:

Rais John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, George Simbachawene, kumkabidhi taarifa ya faida iliyozalishwa na Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (UDART) tangu mradi wa mabasi yaendayo haraka ulivyoanza hadi sasa.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo wakati akizindua miundombinu na utoaji wa huduma ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza , leo jijini Dar es Salaam.

“Mawaziri watueleze hizo pesa mlizotengeneza tangu mradi huu unaanza hadi sasa ili watanzania wajue faida iliyotokana na mkopo wanaolipa kupitia kodi zao,” amesema.

Dkt. Magufuli amesema kuwa, alitarajia kutumia faida itokanayo na mradi wa mabasi yaendayo haraka kujenga maegesho ya gari za watu binafsi pamoja na kituo cha daladala eneo la Kimara mwisho ili kuondoa usumbufu kwa abiria wanaotaka magari ya kawaida pamoja na watu binafsi wanaotoka nje ya jiji kupata nafasi ya kuegesha magari yao.

“Kama ingekuwepo taarifa za fedha hizo ningeagiza ujenzi wa maegesho ya magari ya watu binafsi katika kituo cha Kimara mwisho ili wenye magari binafsi wayaegeshe pindi wanapopanda gari za mwendokasi,”

Aidha, amewaagiza watendaji wa mradi huo kujiendesha kwa faida ili serikali ipate mapato pamoja na kulipa deni ililokopa kutoka Benki ya Dunia zaidi ya bilioni 400 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya mradi huo.

“Huu mradi lazima upate faida, watendaji wajipange kupata faida ikipatikana hasara itakua yao na si ya serikali,” amesema.

Pia amepiga marufuku viongozi wa mradi huo kuanzisha kampuni ndogo ndogo kwa ajili ya kutoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka.

“Msianzishe kampuni ndogo ndogo kama za kukata tiketi, kutoa ajira na kadhalika, nayajua yote hayo kama mnampango wa kuanzisha kampuni,” amesema.

Share:

Leave a reply