JTI yatoa vifaa tiba kwa zahanati ya Usindi wilayani Kaliua, Tabora

407
0
Share:

Kampuni ya Japan Tobacco International (JTI) imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 13.5 kwa Zahanati ya Kijiji cha Usindi wilayani Kaliua kwa ajili ya uboreshaji wa huduma matibabu kwa wakazi wa eneo hilo.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na vitanda vya wagonjwa, vitanda kwa ajili ya wakina mama kujifungulila, darubini za kuchunguzia magonjwa, viti vya wagonjwa na  mizani ya kupimia uzito.

Akipokea msaada huo jana katika Kijiji cha Usindi kwa niaba ya wakazi wake , Mkuu wa Wilaya  ya Kaliua Abel Busalama alisema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuboresha huduma kwa mama wajawazito, huduma za uchunguzi wa magonjwa na kuongeza ufanisi wa kazi kwa wataalumu wa Zahanati hiyo.

Alisema kuwa uwepo wa vifaa utasaidia sio tu kutoa huduma kwa wakazi wa Kijiji hicho pekee hata majirani na wapiti njia ambao watahitaji huduma ya dharura.

Busalama alisema kuwa wakazi wa Wilaya hiyo wamekuwa wakilazimika kutembelea umbali mrefu kutafuta matibabu, kwa hiyo msaada huo utawasidia kuwapunguzia wakazi wa Kijiji hicho kwenda mbali kutafuta huduma za kiuchunguzi.

Aliishukuru Kampuni ya  JTI kwa juhudi zao za kutumia sehemu ya faida wanayopata kutokana na ununuzi na uuzaji wa tumbaku na kuamua kurudisha kwa jamii kwa kutoa misaada mbalimbali inayolenga kuondoa matatizo kwao.

“Ni washukuru sana JTI kwa kuwa hii sio mara ya kwanza kwenu kusaidia jamii mnayoshirikiana nayo …ni hivi karibuni mlikabidhi kisima chenye uwezo wa kuzalisha lita 7000 , hii  ni ishara kuwa mnashirikiana vizuri na wakulima ambapo wafanyia kazi zenu” alisema Busalama.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaliua aliwapongeza viongozi wa Chama cha Msingi cha Usindi AMCOS kwa uaminifu wao ambao kupitia Chama hicho umewezesha Kampuni ya JTI kuamua kutoa msaada kwa Zahanati ya Kijiji hicho.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt. Aristides Raphael alisema msaada huo walioupata utasaidia kuboresha utoaji wa huduma katika Zahanati hiyo na kuahidi  kupeleka mtaalamu wa maabara ili wakazi wa hapo waanze kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa.

Alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia wakazi wa Kijiji hicho kutotembea umbali mrefu kutafuta huduma za uchunguzi wa kimaabara kwa baadhi ya magonjwa na badala yake watapata palepale.

Naye Mwalikilishi wa Kampuni ya JTI Ally Kalugala alisema kuwa vifaa walitoa kwa ajili ya Zahanati ya Usindi ni sehemu ya mpango wao wa kushirikiana na wakulima ambao wamekuwa wakifanyakazi nao katika kuhakikisha kuwa wanashiriki vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Alisema kuwa wataendelea kutoa misaada kwa wakulima ambao wa kijiji cha Usindi na maeneo mengine katika kusaidiana katika utatazi wa matatizo mbalimbali yanawakabili na kupunguza juhudi zao za kujikwamua na umaskini.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Usindi AMCOS Mikidadi Mustapha alisema kuwa wamekuwa na mahusiano mazuri na Kampuni ya JTI na uzalishaji umekuwa ukiongezeka kila mwaka.

Alisema kuwa ushirikiano huo ndio umepelekea kuwa na mazungumzo na Kampuni hiyo kwa ajili ya kuomba msaada wa vifaa ambapo hatimaye wamepatiwa vifaa kwa ajili ya Zahanati ya Kijiji.

Na Tiganya Vincent, Tabora

Share:

Leave a reply