Jumia Travel yatoa tuzo kwa hoteli zinazofanya vizuri nchini Tanzania

361
0
Share:

Mtandao unaoongoza kwa huduma za hoteli kwa njia ya mtandao barani Afrika wa Jumia Travel umetoa tuzo kwa hoteli na washirika wake wakati wa hafla fupi iliyofanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa hoteli ya Mayfair jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo hizo, Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania Bi. Fatema Dharsee alibainisha kuwa tuzo hizo zimelenga kuleta chachu katika matumizi ya huduma za hoteli mtandaoni nchini na kupanua wigo wa huduma kwa wateja.

“Leo hii tumejumuika hapa kuzitambua na kuzitunuku hoteli zinazotoa huduma nzuri pamoja na kupendwa na wateja wa ndani na nje ya nchi. Mbali na sababu hizo lakini kikubwa zaidi ni kwa hoteli hizi kuendana na mabadiliko ya teknolojia kupitia mtandao wa intaneti ambao unawezesha huduma zao kufikiwa na mtu yeyote duniani,” alisema Bi. Dharsee.

1Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee (kulia) akikabidhi tuzo ya Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa mwaka 2016 kwa Meneja wa Huduma za Hoteli ya Amaan Bungalows, Bw. Daudi Fundi (kushoto). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jioni ya siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.

“Hoteli zote zilizojiunga au kujumuishwa kwenye mtandao wetu wa ‘Extranet’ zinazo fursa kubwa za kuongeza ufanisi na thamani ya biashara yao kwani hazitegemei tena wateja wanaokwenda moja kwa moja kutafuta huduma kwenye meza zao za maulizo. Kupitia mtandao wetu ambao unapatikana kwenye kompyuta, tabiti na simu, unamwezesha meneja wa hoteli au mapokezi mahali popote walipo mbali na vituo vyao vya kazi kupokea maombi ya wateja kisha kuthibitisha au kubatilisha upatikanaji wa huduma husika,” aliongezea Bi. Dharsee

Aliendelea mbele kwa kufafanua zaidi kuwa vipengele vya tuzo za Jumia Travel Tanzania vilivyokuwa vikiwaniwa ni pamoja na:

Chaguo la Wasafiri – hii ilitolewa kutokana na maoni ya wateja au wageni wengi walioitembelea; Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa – hii ilitolewa kwa kigezo cha kuthamini mchango na ushirikiano wake; Hoteli Bora Inayochipukia – hii ilitolewa kutokana na juhudi na jitihada zilizooneshwa katika sekta nzima kwa ujumla; Hoteli Iliyopokea Maombi Zaidi Kutoka Kwa Wateja – hii ilitolewa kwa mujibu wa kuwa na maombi mengi kutoka kwa wateja; na Mshirika Bora Katika Biashara – hii ilitolewa kwa kutuunga mkono na mchango mkubwa katika biashara.

“Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa hoteli zote zilizokubali wito na kuhudhuria hafla hii. Uwepo wenu hapa jioni ya leo unaonyesha kutuamini na kuunga mkono jitihada za kuinua sekta ya utalii na ukarimu nchini hususani kuhamasisha kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani,” alihitimisha Meneja Mkaazi huyo wa Jumia Travel nchini Tanzania.

3Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee (kulia) akikabidhi tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara mwaka 2016 kwa Mtendaji wa Mauzo wa Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam, Bi. Emma Sizya (kushoto). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jioni ya siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo hoteli zilizojinyakulia tuzo hizo ni pamoja na Serena ambayo ilitunukiwa tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara; Tanzanite Executive Suites ilitunukiwa tuzo ya Chaguo Bora la Wasafiri; Amaan Bungalows ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa; Harbour View Suites ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyopokea Maombi Zaidi Kutoka Kwa Wateja; na Slipway ambayo yenyewe ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Bora Inayochipukia.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo Mtendaji wa Mauzo kutoka hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam Bi. Emma Sizya amesema kuwa amefarijika kupokea tuzo hiyo na kuipongeza kampuni ya Jumia Travel Tanzania kwa kuja na kitu hiki cha kipekee.

5Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu kampuni katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa hoteli zilizofanya vizuri mwaka 2016 mbele ya wageni waalikwa na waandishi wa habari (hawako pichani). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jioni ya siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.

“Kwanza ningependa kuipongeza Jumia Travel Tanzania kwa kuja ni hizi tuzo ambazo ninaamini kuwa zitaleta mchango mkubwa katika kuhamasisha sekta ya hoteli nchini. Tumekuwa tukiona sekta mbalimbali zikiwa na tuzo zao lakini yetu ikiwa imelala kidogo, huu ni mwanzo mzuri na ninaamini waandaaji hawataishia hapa,” alisema na kumalizia Bi. Sizya kwamba, “Serena siku zote tunajivunia kuwa mbele katika kuunga mkono jitihada za wadau mbalimbali wanaofanya kazi na sisi. Lengo letu kubwa ni kuona kuwa kwa pamoja tunashirikiana katika kuwashawishi wateja kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ambapo sasa hivi kupitia kampuni kama hii unaweza kupata huduma zetu mtandaoni.”

Hafla hiyo imeambatana na kuadhimisha miaka mitatu tangu Jumia Travel kuanzishwa pamoja na kampeni maarufu ya mauzo inayoendelea kwa jina la ‘Black Friday’ ambayo  imeanza Novemba 14 mpaka Novemba 25, 2016. Matarajio ya kampuni kwa wiki hizi mbili za mbili ni makubwa ambapo imelenga kuwapatia wateja fursa ya kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma za awali kwa ajili ya msimu wa sikukuu kwa gharama nafuu.

6Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Bi. Fatema Dharsee akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa hoteli zilizofanya vizuri mwaka 2016 mbele ya wageni waalikwa na waandishi wa habari (hawako pichani). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jioni ya siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.  

Share:

Leave a reply