Kamanda Sirro awaonya madereva wanaokatiza njia za reli

470
0
Share:

Kufuatia ajali iliyotokea leo Aprili 19, 2017 maeneo ya Gold Star jijini Dar es Salaam, majira ya saa 11.30 alfajiri, ambapo Basi la Gongo la Mboto lenye namba T434 DGG liligonga treni ya Pugu na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi wapatao 27.

Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro amewataka madereva kutii sheria za barabarani bila shuruti pamoja na kuwa makini wawapo kwenye njia za reli ili kuepukana na ajali pamoja na kulinda usalama wa abiria.

Kamanda Sirro ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa hadi sasa majeruhi 15 kati ya 27 wameruhusiwa kutoka hospitalini huku 12 wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Amana.

” Gari hadi sasa lipo maeneo ya Rail way, ila niwakumbushe madereva kutii sheria bila shuruti, pia kuwa makini wanapokuwa kwenye njia ya reli ili kulinda usalama wa raia,” amesema.

Wakati huo huo: Kamanda Sirro amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa 267 kwa makosa mbalimbali ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, utapeli, wizi, kucheza kamari, na kupatikana kwa dawa za kulevya,  kuanzia Aprili 13 hadi 17,2017.

Akieleza tukio hilo, amesema takribani kete 366 za dawa za kulevya, bhangi misokoto 51 na lita 200 za pombe haramu aina ya gongo zilikamatwa kufuatia operesheni kali iliyofanywa na askari polisi.

“Pia Polisi wamekamata watuhumiwa watatu kwa wizi wa vitu mbalimbali maeneo ya Chamanzi wanaofahamika kwa majina ya Athuman Bashiru na Rashid Seleman na Mohamed Mussa. Pia wamekamata pikipiki moja ya wizi na kwamba watuhumiwa wawili wanashikiliwa kufuatia tukio hilo ambapo walimkata na panga kichwani mmiliki wake Ibrahim Shaban na kumpora pikipiki hiyo,” amesema.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi mnamo Aprili 10, 2017 limekamata watuhumiwa watano wa ujambazi ambao hushirikiana kufanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Salimu Matanda, Eliaki Chaki, Shaban,  Rashid Said, na Nassoro Choro ambao wamekamatwa baada ya kuiba pikipiki aina ya Boxer inayomilikiwa na Noel Mkinga.

Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi lilikamata silaha moja aina ya Shotgun maeneo ya Kiwalani iliyofutwa namba za usajiri baada ya wahalifu waliokuwa nayo kuitekeleza walipokuwa wanakimbizwa na Polisi.

Share:

Leave a reply