Kampuni ya Elite kutoa misaada kwa wanawake waishio Mabwepande

188
0
Share:

Kutokana na hali ya kimaisha kwa wananchi ambao wanaishi eneo la Mabwepande, Kampuni ya Elite Organizers Service imefanya uzinduzi wa kampeni ya Declutter&Donate ambayo inalenga kuwasaidia wanawake wanaoishi eneo hilo ili kuwapatia msaada wa taulo za hedhi (pad).

Akizungumzia kampeni ya Declutter&Donate ambayo imezinduliwa Jumanne ya Septemba, 13, Mwanzilishi wa kampuni ya Elite Organizers Service, Nasra Karl Mbululo alisema kuwa kampeni hiyo imezinduliwa mahsusi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto yatima.

Alisema kampeni hiyo itahusika na kukusanya vitu ambavyo havitumiki nyumbani na maofisini na kisha vitauzwa na baadae watakwenda kutoa taulo za hedhi kwa wanawake 814 ambao wanaishi eneo la Mabwepande.

Kwa upande wa watoto yatima, Nasra alisema kuwa watakusanya vitabu na midoli kutoka kwa watu mbalimbali ambao watakuwa tayari kujitolea na baadae watapeleka katika moja ya kituo ambacho watakichagua.

Mwanzilishi wa kampuni ya Elite Organizers Service, Nasra Karl MbululoMwanzilishi wa kampuni ya Elite Organizers Service, Nasra Karl Mbululo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya Declutter&Donate ambayo inalenga kuwasaidia wanawake na watoto yatima.

“Kuna vitu tunakuwa navyo majumbani kwetu au ofisini na hatuvitumii, hivyo vitu sisi tunaviomba na tutakwenda kuviuza na kuwagawia wanawake waliopo Mabwepande, ukiangalia mazingira ambayo wanaishi wengine nyumba zao hata bati hawana kwahiyo kutumia pesa kununua pad (taulo za hedhi) anaona bora anunue chakula au kuongeza ili ajenge kwahiyo sisi tutawapa pad ili kupunguza gharama,

“Pamoja na hilo pia tutakuwa tunachukua na vitabu na toys (midoli) ambayo majumbani hawaitumi na sisi tutakusanya vitu hivyo na kwenda kuwagawia watoto yatima kwenye kituo cha kulelea,” alisema Nasra.

Aidha alisema kuwa, watatoa mafunzo kwa wanawake wa Mabwepande ambayo yataongozwa na Mshauri Mwandamizi wa Life Style, Sadaka Gandi ambaye atawapa mafunzo wanawake hao kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu afya.

Pia alisema kuwa hivi karibuni watatangaza vituo ambavyo vitatumika kukusanya vitu ambavyo vitakuwa vinatolewa na hivyo kwa yoyote ambaye ataguswa na kampeni hiyo atakuwa akipeleka msaada wake katika vituo hivyo.

Share:

Leave a reply