Kampuni ya matangazo ya Kwanza yatangaza neema kwa watangazaji na wachapishaji

324
0
Share:

Mtandao wa Kwanza Advitising Network imezindua jukwaa la utangazaji bidhaa linalokutanisha kampuni mbalimbali na wachapishaji wa mtandaoni ikiwemo blog na mitandao(Website) kwa ajili ya kutangaza bidhaa mtandaoni.

Akifafanua wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo, Meneja Uzalishaji kutoka Kwanza Advitising Network, Leon John ameeleza namna ya jukwaa hilo litakavyofanya kazi ambapo mtandao huo utaunganisha kampuni za uzalishaji, wachapishaji mtandaoni na wateja.

“Mtandao wetu utawakutanisha wachapishaji wa mtandaoni na kampuni za uzalishaji ambazo zitakua zinatangaza bidhaa zao, mfano kampuni za simu, usafirishaji na kadhalika,” amesema.

Naye Meneja Mawasiliano Kwanza Advitising Network, Herman Mkamba ameeleza vigezo vitakavyotumika kuchagua mitandao na blog zitakazo jiunga kwenye jukwaa hilo, ambapo kigezo cha kwanza mtandao unatakiwa kuwa na idadi kubwa ya watembeleaji na kuwa na vyanzo vya uhakika vya taarifa.

“Wachapishaji watalipwa kulingana na idadi ya watembeleaji wake,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Mtandao wa Blog nchini,Krantz Mwantepele amesema jukwaa hilo litasaidia wamiliki wa blog kupata kipato, na kuwataka wamiliki hao kuandika habari za uhakika ili watengeneze watembeleaji wengi.

Meneja wa Masoko ya Digitali kutoka kampuni ya simu za mkononi TECNO ambayo ni miongoni mwa kampuni zilizomo kwenye jukwaa hilo, Kelvin Boniface amesema jukwaa hilo litasaidia kampuni kutangaza bidhaa zao kwa wateja kwa haraka.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply