Kesi za migogoro ya kazi kuanza kusikilizwa Oktoba 16

398
0
Share:

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania – Divisheni ya Kazi, Mhe. Hellen Mkubwa amesema kwamba watendaji wa Mahakama ya Tanzania, wataendelea kushirikiana na wadau wa Mahakama ili kuweza kumaliza mashauri yaliyopo Mahakamani yanayohusu migogoro ya kazi kwa haki na wakati. 

Aidha Bi. Hellen alisema hatua ya kuwawezesha wananchi kupata haki zao kwa wakati ikiwa ni hatua ya kutatua changamoto zilizopo, mfano vile za ucheleweshaji wa majalada , upungufu wa vitendea kazi na uhaba wa rasilimali watu. 

Kauli hiyo ilitolewa na Mtendaji huyo, wakati wa kikao cha Maandalizi ya Kikao cha Mashauri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam jana. 

Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili jinsi ya kuweza kusikiliza kesi, kulingana na Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano wa 2015/2016 hadi 2019/2020 , ili kuwawezesha kupata haki zao kwa wakati, hatimaye waweze kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ya nchi na kukuza uchumi wa taifa. 

Mtendaji huyo alitoa kauli hiyo , baada ya Naibu Msajili Mfawidhi kuelezwa na kwamba moja ya changamoto za usikilizaji wa kesi hizo ni ucheleweshaji ya majalada kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi( CMA). 

Kikao hicho cha kusukuma mashauri ya muda mrefu kinatarajiwa kuanza kusikilizwa kuanzia Oktoba 16 hadi Novemba 17 mwaka huu katika mikoa mbalimbali Nchini. 

Aliitaja mikoa hiyo vikao vya mashauri vitafanyika katika mikoa ya Mwanza, Bukoba, Musoma, Sumbawanga,Mbeya, Iringa, Dodoma,Musoma, Bukoba, Morogoro, Lindi, Mtwara, na Kigoma. 

Alisema hukumu za kesi, hizo zitaanza kutolewa kuanzia Novemba 3 hadi 17 mwaka huu. Bi. Hellen aliongeza kwamba kuna jumla ya mashauri ni 674 yaliyopangwa kusikilizwa na majaji watano pamoja na wasajili watatu. 

Katika kikao hicho, mmoja wa washiriki hao kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi( CMA) , Kaimu Naibu Mkurugenzi , Bw. Emily Mwidunda, ambaye pia ni Makamu alisema changamoto, iliyopo katika kushughulikia mashauri hayo ni uhaba wa vitendea kazi mfano wana kompyuta 23 na idadi ya kompyuta zinazohitajika zinazohitajika ni 80. 

Pia Tume ya CMA wana changamoto makatibu Mahsusi, waliopo ni wachache na hii inapelekea kuzidiwa kwa kazi na haki kuchelewa kupatikana kwa wakati. 

Kikao hicho kimejumuisha baadhi ya wadau wafuatao, ambao ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Chama cha Waajiri Tanzania ( ATE), TUICO, Wakilishi Binafsi, (Tutse) ,( Chama cha Wafanyakazi na Kampuni za Walinzi, Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG ), na Mawakili wa kawaida.

Na Magreth Kinabo, Mahakama ya Tanzania

Share:

Leave a reply