Kongamano la masuala ya petroli Afrika Mashariki kufanyika Kenya 2019

117
0
Share:

Kongamano na Maonesho ya Tisa ya masuala ya Petroli kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanatarajiwa kufanyika nchini Kenya, Machi 2019.

Azimio hilo limepata baraka za Mkutano Ngazi ya Makatibu Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika Kampala, Desemba 1, mwaka huu.

Mkutano huo wa Makatibu Wakuu ni maandalizi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wenye lengo la kupitia nyaraka na taarifa za Maandalizi ya Mkutano wa Kazi wa Wakuu wa Nchi kabla ya kuziwasilisha kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliopangwa kufanyika mwezi Januari, 2018.

Kuteuliwa kwa Kenya kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo kubwa, kunatokana na mzunguko wa kawaida wa ratiba yake, ambapo makongamano yaliyotangulia yalifanyika katika nchi za Jumuiya husika kwa mlolongo wa Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Hivyo basi, kutokana na mzunguko huo, Makatibu Wakuu wamebariki, Kongamano lijalo lifanyike Kenya kuanzia tarehe 6 hadi 8 Machi, 2019.

Aidha, Mkutano huo pia uliazimia kuwa, maandalizi ya Kongamano husika yaanze mapema ili kuwepo muda wa kutosha wa kujitangaza na kuvutia ushiriki wa mataifa mbalimbali duniani.

Masuala mengine yahusuyo nishati, yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na maendeleo ya upembuzi yakinifu kwa Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Kigali hadi Bujumbura, Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Mbarara – Mwanza – Isaka hadi Dar es Salaam, pamoja na kuoanisha mfumo wa kisheria na udhibiti wa masuala ya nishati.

Vilevile, Mkutano huo pia ulijadili maendeleo endelevu ya Kituo cha Ubora (Centre of Excellence) cha masuala ya Nishati Jadidifu na Matumizi Bora ya Nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichopo kwenye Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda.

Mbali na masuala ya nishati, sekta nyingine zilizojadiliwa katika Mkutano huo ni elimu ya juu, miundombinu, uchukuzi, fedha pamoja na afya.

Tanzania, kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine wanachama, iliwakilishwa na wataalam mbalimbali kutoka sekta husika pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua.

Na Veronica Simba, Kampala

Share:

Leave a reply