Kusupa awakumbusha waandishi wa habari majukumu yao kwa jamii

217
0
Share:

Kufuatia mvutano wa kisiasa unaoendelea baina ya serikali na vyama vya siasa vya upinzani nchini, vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari wametakiwa kuitumia taaluma yao kuandika habari zitakazosaidia mvutano huo kuisha na si kuandika habari zinazouchochea mgogoro huo.

Hivi karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza adhma yake ya kufanya mikutano ya kisiasa nchi nzima ifikapo Septemba1,2016 huku serikali ikikataza kufanyika mikutano hiyo kwa madai kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kutokana na migongano hiyo, Mwandishi wa habari mwandamizi, Kamara Kusupa amevitaka vyombo vya habari kuacha Ushabiki na kuishauri serikali.

“Ipo haja kwa waandishi kwenda ndani zaidi ili kuishauri serikali pamoja na vyama vyama vya siasa kukaa pamoja na kuzungumza namna ya kuumaliza mgogoro huo ili usijeleta madhara kwa jamii,” amesema Kusupa.

Amesema sasa ni wakati wa waandishi kuishauri serikali jinsi ya kuutatua mgogoro huo na si kuripoti habari kulingana na ushabiki.

“Kuna mgogoro kati ya Chadema na serikali ni vema waandishi wakaandika mawazo yatakayoondoa mgogoro huo na si kuandika habari zenye mtizamo hasi,” amesema.

“Magufuli ameshika dola na ina Makali, vyama vya upinzani ni sawa vimeshika Malawi huku rais akishika mpini, hivyo kama pande hizi mbili hazitakaa pamoja hakutakuwa na suluhisho la kudumu,” ameongeza.

Ameeleza kuwa si Jambo rahisi vyama vya upinzani kuacha kufanya mikutano itakayowawezesha kukutana na wananchi kwa kuwa mikutano ndiyo njia sahihi ya kupata wanachama wapya.

“Hakuna jinsi pande zote mbili zikae pamoja ili muafaka upatikane,” amesema.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply