Lipumba ang’oa wakurugenzi wanne wa Maalim Seif

543
0
Share:

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba leo ametengua uteuzi wa wakurugenzi watano ambao ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya chama hicho kutoka Zanzibar. Kwa madai ya kutoitikia wito wa kuhudhuria kikao cha kamati hiyo Machi 6, 2017 kilichoitishwa na Naibu Katibu Mkuu Bara wa CUF, Magdalena Sakaya.

Wakurugenzi waliodaiwa kutenguliwa uteuzi wao ni pamoja na, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Omar Shehe, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma Salim Bimani, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi Abdallah Hassan,Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria Pavu Abdallah na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Vijana CUF (JUVICUF)  Mahmoud Mahinda.     

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa tamko la kutengua uteuzi wa wakurugenzi hao, Prof. Lipumba amedai kuwa atateua wakurugenzi wengine kabla ya wiki hii kuisha, ili Sakaya aitishe kikao kingine cha kamati kuu ya utendaji kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi.

Licha ya kutengua uteuzi wa wakurugenzi hao, Lipumba amedai kumuweka kiporo Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar Nassoro Mazrui kwa madai ya kutotoa ushirikiano kwa Naibu Katibu Mkuu Bara licha ya kutambua kwamba ni kiongozi wake halali kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

“Sakaya amewatumia ujumbe wa simu wakurugenzi wote wa Tanzania Bara wamehudhuria mwengine alikuwa na ziara na Rais John Magufuli Mtwara lakini aliaghirisha akaja, kitendo cha wengine kutofika baada ya kupewa taarifa, siwezi kukubali. Sakaya namuagiza mimi halafu wakurugenzi hawaji na hawatoi taarifa yoyote? lazima wawe tayari kufanya kazi na katibu mkuu na manaibu katibu mkuu wote,” amesema Lipumba.

MO BLOG ilimtafuta mmoja wa wakurugenzi aliyedaiwa kuvuliwa madaraka yake, na kufanikiwa kumpata Mkurugenzi wa Habari  Salim Bimani ambaye alidai kuwa yeye pamoja na wenzake hawatambui maamuzi hayo ya Lipumba kwa madai kuwa si mwenyekiti halali kwa mujibu wa katiba ya CUF kwa kuwa alijiudhuru sambamba na kufutwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho.

“Hana uwezo wowote wa kututengua na hatumtambui, kwanza kuna kesi mahakamani hivyo kila analolifanya ni batili hadi pale mahakama itakapo toa maamuzi yake. Kwa sasa tunachofahamu ni kwamba anafanya maamuzi kwa masilahi yake binafsi,” amesema Bimani. 

Share:

Leave a reply