Lipumba awaonya wakurungezi aliowatengua kutoendelea kufanya kazi

751
0
Share:

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amewaonya baadhi ya  wakurugenzi aliodai kutengua teuzi zao kutoendelea kufanya kazi za wakurugenzi wa chama hicho kwa kuwa ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu cha 8B (2).

Lipumba alitoa onyo hilo Machi 12, 2017 katika Ofisi Kuu za chama hicho, wakati akitoa taarifa ya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji CUF. Licha ya kutoa onyo, Lipumba amesema hatovumilia baadhi ya viongozi wanaokigawa chama hicho kwa misingi ya ubara na uzanzibari.

“Nawaonya wale niliotengua ukurugenzi wao wasiendelee kujitangaza na kufanya kazi za ukurugenzi wa chama. Wakifanya hivyo wanakiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 kinachoeleza kuwa mtu yeyote ambaye sio kiongozi wa chama haruhusiwi kufanya shughuli yoyote kama kiongozi wa chama hicho. Mtu yeyote anayevunja kifungu hiki cha sheria anafanya kosa la jinai,” alisema na kuongeza.

“Hivi sasa kuna dalili ya viongozi wanaokigawa chama, nasisitiza mimi kama mwenyekiti wa Taifa wa chama sitawavumilia watu hao na nitakua ngangari kupambana nao sababu uhatarisha muungano wetu kwa mikakati ya kukigawa chama. Na nilioteua leo hawakubali kukigawa chama wana dhamira ya dhati ya kusimamia haki sawa.”  

Wakurugenzi walioteuliwa na Lipumba ni pamoja na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Nassor Seif, Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi Haroub Shamis, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano Masoud  Said,pia amemteua Abdul Kambaya kuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi.

Baada ya uteuzi huo, Lipumba alimuagiza Naibu Katibu Mkuu Bara , Magdalena Sakaya kuitisha kikao cha Kamati ya Utendaji ambacho kinafanyika leo kwa lengo la kuandaa mipango ya chama.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply