Maalim Seif adai Prof. Lipumba anatumika kuzima mgogoro wa uchaguzi Zanzibar

825
0
Share:

Licha ya mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) kufikishwa mahakamani na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho hivi karibuni kufungua shauri namba 23/2016 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake kwa madai kuwa wadaiwa hao wanashiriki kuihujumu CUF.

Bado mgogoro huo unaendelea ndani ya CUF kuanzia ngazi ya kata hadi taifa, ambapo viongozi waandamizi wa chama hicho ambao ni Katibu Mkuu Maalim Seif Sherif Hamad na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho aliyefutwa uanachama, Prof. Lipumba wameendelea kupeana tuhuma na kwamba kila mmoja anamtuhumu mwenzie kuwa na ajenda ya kukihujumu chama hicho ili kivunjike kitendo kilichosababisha wanachama na viongozi wa chama hicho kugawanyika.

Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesema kuwa yeye sio sababu ya mgogoro uliopo sasa na wala hajahusika kumfukuza uanachama Lipumba bali CUF kupitia Baraza lake la Uongozi Taifa liliamua kumfuta uanachama kwa sababu ya kukiuka katiba ya chama hicho.

“Sina ugomvi na Lipumba, sijamfukuza, na niko radhi kufanya nae mdahalo ili aeleze siri ya kujiudhuru na kung’ang’ania uenyekiti wa CUF. Na hata tukipatanishwa haitasaidia kitu sababu, siwezi badilisha, chama ndicho kilichomfukuza kwa kura za wajumbe zaidi ya asilimia 70,” amesema.

Maalim amedai kuwa, Lipumba anatumiwa na baadhi ya watu kuuzima mgogoro wa uchaguzi uliotokea visiwani Zanzibar mwaka jana.

“Mgogoro huu wa CUF ni muendelezo wa hujuma zinazohusiana na kuzima harakati za kudai haki Zanzibar, ndio maana Lipumba analindwa na vyombo vya dola kuuendeleza mgogoro huu ili CUF ishindwe fuatilia mgogoro wa uchaguzi Zanzibar na kwamba wakubwa waonekane hawakukosea,” amesema.

Licha ya Maalim kumtuhumu Lipumba kutaka kuisambaratisha CUF, Jumamosi ya Novemba, 26 Prof. Lipumba katika mkutano wake wa ndani na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ya CUF wilaya ya Temeke, alidai kuwa Maalim na wafuasi wake wanapanga mikakati ya kukiuza chama na kwamba anahonga baadhi ya viongozi wa CUF kuanzia kata ili wamkatae kwa madai kuwa yeye ni kikwazo kwa Maalim kukiuza chama hicho.

Hata hivyo, Maalim amemjibu kuwa “Anasema nakiuza chama kwa Ukawa na Chadema, au Lowassa, anasahau kuwa yeye ndio aliyekuwa anasema amezunguka mitaani na kugundua kuwa wananchi wanamtaka Lowassa hivyo aunganishwe nae ili amsihi ahamie Ukawa, leo hii anasema nataka kuuza chama, yeye na mimi nani aliyekuwa na nia ya kumkaribisha huyo mtu anayenituhumu kuwa nataka kumuuzia chama?”

Aidha, Mgogoro wa CUF ulianza pamba moto wakati Prof. Lipumba na baadhi ya wafuasi wake walipovamia makao makuu ya ofisi za chama hicho baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutamka kumtambua kama mwenyekiti halali wa CUF.

Hata hivyo, mgogoro huo umesababisha baadhi ya viongozi wa CUF wa wilaya waliopo upande wa Lipumba hasa Makatibu wa Wilaya kupanga njama za kukwamisha shughuli za kichama za Maalim Tanzania Bara hadi pale atakapo tamka kwa kinywa chake kuwa Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply