Makala: Mambo usiyoyajua kuhusu UFOs (Unidentified Flying Objects)

957
0
Share:

Katika Dunia tuishiyo sasa binadamu hatuko peke yetu, lakini tumejijengea dhana kuwatunaishi peke yetu huku tukisahau kuwa Mungu kaumba viumbe kadha wa kadha vinavyoonekana na visivyoonekana.

Unaweza kushangaa ama kudhani kuwa namaanisha juu ya uwepo wa nguvu za kigiza, La Hasha!, mtu anapokuuliza kwamba Je unafahamu maana ya neno ‘UFO’ (Unidentified Flying Object)? Bila shaka watu wengi watakuwa hawafahamu kuhusiana na vitu hivi na wengine wanaweza kukupa maana nyingine tofauti na mada.

Neno UFO limechukua kasi kwenye vyombo vya habari vingi duniani hasa vya wenzetu wa nchi za Magharibi, pia upande wa Asia ambapo baadhi ya Wataalam wamajaribu kufuatilia kwa karibu juu ya vitu hivi na wapi vimetokea na madhumuni ya kuonekana ovyo katika maeneo tofauti na madhara yake lakini hakuna maelezo mazuri yanayoweza kuelezeka katika hilo, na hii imepelekea wataalam hao kuziita baadhi ya tafiti zao kuwa ni zisizoelezeka (Unexplained files about UFOs)

Ebu tujiulize maswali UFOs ni vitu gani, na malengo yake kuonekana duniani ni nini haswa?

UFOs ni Vyombo vyenye ukubwa tofauti na maumbile tofauti ambapo vingine vinakadiliwa kuwa na ukubwa wa futi 100 ama zaidi vingine na muonekano wake ni wa duara kama sahani kubwa la chuma lenye kung’aa (steel shaped-saucer), lakini pia vinaweza kuwa na umbo mengine tofauti kama vile maumbile ya pembe tatu ambapo kwa chini zinakuwa ya na taa zenye kutoa miale mikali ya mwanga yenye rangi ya bluu, nyekundu na nyeupe.

UFOs ndizo zinabeba viumbe wajulikanao kama Aliens na viumbe hawa wanamaumbo kama ya binadamu lakini tofauti yake iko katika macho na vidole kwani viumbe hawa wana macho makubwa yenye umbo la ovali, vidole vikubwa vitatu badala na wakati mwingine mikono mirefu, na miili yao ni kama yenye hali ya mpira hivi na wakati mwingine waonekanapo wanakuwa kama waliovalia aina ya kama nguo zenye kubana mwili mzima zenye rangi ya bluu na mikanda viunoni mwao, hakika viumbe hivi vinatisha kimuonekano wao.

Taarifa zisizo rasmi kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari na maelezo ya watafiti mbalimbali ulimwenguni vinaeleza kuwa UFO hutumika kama chombo cha anga cha kusafiria kwa viumbe hao ambao wanasemekana kutoka katika sayari ya mbali na ni viumbe wenye akili kuliko binadamu wa kawaida.

Vyombo hivi viko tofauti na vyombo vyetu vya anga kama vile ndege za abiria au roketi ziendazo mwezini, kwani tofauti iliyopo hapa ni kwamba vyombo hivi vibebavyo viumbe hao vinasemakana kuwa na kasi ya ajabu tofauti na kifaa chochote cha hapa duniani kuwa na mwendo kasi kama huo, lakini pia UFO CRAFTS zinaweza kubadili mwelekeo wake katika nukta yoyote ya safari yake wakati wowote na kuweza kutoweka machoni ndani ya sekunde.

UFO pindi zifikapo katika uso wa dunia hazitoagi kelele na zinatabia ya kuacha nguvu fulani ya umeme wenye usumaku (Electromagnetic Radiation) ambayo wakati mwingine inaweza kusababisha hitilafu ya umeme wa kawaida tuutumiao, maajabu mengine ni kwamba pindi vikiwa vimetua sehemu fulani basi mfumo mzima wa mawasiliano kama vile ya simu, rada, na wakati mwingine majira ya saa zetu huathiriwa na kwenda kinyume (anticlockwise) na endapo umeme utokanao na nguvu ya usumaku ikiwa iko juu basi moto unaweza kujiwakia popote iwe ndani ya nyumba zetu ama nje hata kwenye maji pia.

Tukio kama hili liliwahi kutokea mnamo Januari 2004 nchini Italia katika kijiji cha Canneto (Caronia) ambapo nyumba za watu zikiwemo samani zao zikiwaka moto licha ya umeme katika kijiji hicho kuzimwa, bado ulizidi kushika kasi na ulikuwa ukiwaka wenyewe toka nyumba moja kwenda nyingine, runinga, friji, majiko yalikuwa yakiwaka moto bila kuwashwa, pia mifumo ya simu nayo haikuweza kufanya kazi, mifumo ya magari ilikuwa ikijiwasha na kujizima yenyewe bila kuwashwa pamoja na honi za magari zikijipiga zenyewe, ama kweli haya yalikuwa ni maajabu katika eneo hilo ambapo baada ya uchunguzi wa  muda mrefu uliogharimu fedha nyingi na Wataalam wengi ilikuja kubainika kuwa Aliens ndiyo chanzo kikubwa cha moto katika kijiji hicho.

Katika baadhi ya matukio yanayohusiana na uwepo wa UFOs, watu ambao wamekuwa wakisafiri na magari yao pindi wakutanapo na vitu hivyo basi magari yalizimika papo hapo na kushindwa kuwaka na wakati mwingine katika nyakati za usiku, miale ya taa za magari yao ilipinda ghafla na kuelekea katika eneo ambalo UFO imetua lakini hii yote inatokana na nguvu zisizo za kawaida kutoka katika UFOs.

Je, kuna ukweli wowote juu ya madai ya uwepo wa UFOs?

Asilimia 72 ya wananchi wa Marekani wanaamini juu ya uwepo wa uhai nje ya Dunia na kwamba kuna viumbe wengine wanaishi huko. Baadhi yao wanaamini juu ya uwepo wa UFOs na huku wengine ambao ni wahanga wanaamini kuwa wamewahi kukutana nazo katika mazingira tofauti. Kuna wengine pia wanamadai kuwa wao wamewahi kutekwa na viumbe hao (alien abductions) na kuingizwa kwenye UFO na baadaye kurejeshwa walipo kuwa.

Baadhi ya watu ambao wanatoa madai ya kuwahi kutekwa na Aliens, wengi wao wanasimulia kuwa mara walipokutana na UFOs njiani walijikuta ghafla wakiota ndoto na mara wakajikuta wako katika eneo wasilolijua na kulazwa katika vitu kama vitanda na kuchunguzwa na viumbe hao, lakini wengine wamekuwa wakiugua vichwa kwa muda wa wiki nzima pindi walipokutana na aliens huku wengine wakipoteza kumbukumbu kwa muda wa wiki moja na baadaye kurejea katika hali zao za kawaida.

Tarehe 18 Aprili, 1961 Eagle River Wisconsin nchini Marekani, Mkulima na Mfugaji ajulikanaye kama mzee Paul Simonton aliwahi kuona kitu chenye umbile la Sahani kubwa la chuma (UFO) ambayo ilitua katika shamba lake mara juu ya chombo hiko pakafunguka, wakati hayo yakitokea, mzee huyo aliamua kuisogelea kuona ni kitu gani haswa kikiendelea na hapo ndipo akaviona viumbe vitatu vyenye maumbile kama ya binadamu vilionekana vikihitaji maji ndipo yule mzee akachukua jagi lenye maji na kuwapa wale viumbe, cha ajabu nao wale viumbe wakampatia vipande vinne vya keki (4 pancakes) ambavyo hapo baadaye baada ya uchunguzi wa Maabara ilibainika kuwa vipande vile vilitengenezwa kwa kutumia mafuta mazito yaani grisi na unga usiojulikana na usio na radha, tukio hili lilikuwa la ajabu kutokea nchini humo.

Kumekuwepo pia na taarifa lukuki juu ya uwepo wa UFOs kutoka kwenye mitandao mablimabli, magazeti, majarida, kutoka kwa watu waliowahikuona UFOs, walio waona Alliens, mpaka wale waliowahi kutekwa na kuwekwa kwenye UFO Crafts madai haya yote wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuyathibitisha, kwani muda mwingine taarifa hizi zinakuwa kubwa kushinda tukio lenyewe, wakati mwingine kwa makusudi zinakuwa ni taarifa za kutengeneza (propagandas) au zenye upotoshaji kwa umma, lakini bado kuna wakati tukio moja linakuwa na mashahidi zaidi ya mmoja, linakuwa limeacha ushahidi wenye kuonekana yaani ushahidi unaoweza kuugusa kwa mkono, ushahidi ambao ni zaidi ya maneno ya shuhuda mwenyewe.

Hivyo, Katika historia ya vitu hivi na maajabu yake UFOs kwa wanahistoria zinasemakana kurekodiwa kwenye majalada ya historia tangu enzi na enzi ya historia ya mwanadamu, ingawa suala hili halipo kwenye mitaala ya somo la historia lenyewe, na hivyo baadhi ya watu huamini kuwa hakuna kitu kama hicho.

Kuanzia mwaka 1991 mpaka 1993 jiji la Mexico lilifunikwa na taarifa za kuonekana kwa UFOs ukiwemo mwezi wa Julai 11, 1991 ambapo watu 17 ambao hawana mahusiano yoyote katika maeneo tofauti ya jiji hilo wakiwa na kamera zao, waliweza kunasa picha ya sahani kubwa lenye mnga’o wa chuma karibu kabisa na usawa wa jua mbalo muda mfupi nyuma lilikuwa limepatwa na mwezi. Diski hilo lilikuwa limening’inia angani kwa muda bila kusogea upande wowote ule. Lakini watu hawa hawakujua kama wamepiga picha UFO mpaka watu wengine walipo ng’amua wakati wanaonesha video hizo.

Baadaye baadhi ya Watafiti ndipo wakaanza kupokea video na picha nyingi zinazo onesha umbo la duara kubwa la chuma (UFO) zikiwa kwenye anga la Mexico ambazo picha zake zilipigwa na watu tofauti. Vyombo vya rada na hata marubani kadhaa wamewahi kuripoti ama kuviona vyombo hivyo vikiruka katika anga la Mexico. 

Kutoka kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa (Benito Juárez International Airport) Machi 4-5, 1992 tukio la kuonekana kwa UFO liliwahi kuripotiwa na kuthibitishwa na rada ya uwanja huo juu ya kuonekana kwa vitu hivyo.  

Mexico imekuwa na historia ndefu ya kuonekana kwa UFOs na nyingi kati ya hizo zimekuwa zikidharauliwa na wana sayansi huku wakisema kuwa ni vipande vya uchafu ama vumbi kutoka kwenye anga, roketi za kivita, maputo ya hali ya hewa ama uzushi.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati mwingine UFOs vilikuwa vikifukuzwa na ndege ya doria baada ya kudhaniwa kuwa ni ndege za wabeba dawa za kulevya, lakini ghafla ziliweza kutoweka na zilipo onekana tena zilikuwa zimeizingira ndege hiyo ya doria ya jeshi la anga la Mexico.

Mtafiti kwenye masuala ya UFOs, Bwana Brit Elders anazungumzia suala la UFOs kunaswa kwenye rada kwenye jiji la Mexico, “Rada ya Mexico imefuatilia na kurekodi UFO sawa na yale yanayosemwa na watu waliowahi kuona kwa macho yao wenyewe kutoka ardhini na kutoka kwa marubani wa ndege wakiwa angani”, alisema Elders.

Katika tukio hilo, Serikali ya Mexico iliposhinikizwa na wadau mbalimbali juu ya kulifanyia uchunguzi suala tukio hilo ambapo Serikali hiyo ilifanya mkutano na waandishi wa habari na kufafanua kuwa, Serikali hiyo ilitambua juu ya kuonekana kwa vitu hivyo lakini ikasisitiza kuwa UFOs hazina madhara yoyote kwa wananchi.

Tukio jingine la mwezi Machi 13, 1997 katika Jimbo la Arizona kwa dakika 106 mida ya saa mbili na robo usiku lilishuhudia kile ambacho baadaye kilijulikana kama ni UFO. Baada ya tukio hilo simu zilimiminika kwenye vituo vya dharura vya jimbo hilo kutoka kwa mashuhuda wa  maeneo kadhaa ikiwemo Prescott, Wickenburg, Glendale, Phoenix, Scottsdale na Tempe.

Kutoka kwa mashuhuda hao, ni kuwa chombo hicho kilikuwa karibu kabisa na kituo cha Luke Air Force, ambapo ndege aina ya Falcon Super Hornets (F-16) tatu zilitoka kwenda kufuatilia chombo hicho kujua ili kuweza kujua kulikoni, lakini ndege hizo za kijeshi mara zilipokaribia chombo hicho kilitoweka ghafla kama kupepesa mboni ya jicho. Hata hivyo baadhi ya maafisa wa kituo hicho cha Luke kama ilivyo tegemewa walikataa kuwa hakuna ndege za kijeshi zilizotolewa kwenda kukifuatilia chombo hicho na wala hawafanyi tafiti juu ya uwepo wa UFOs.

Peter Davenport toka Kituo cha Taifa cha kutoa Taarifa za UFOs kilichopo Seattle, Washington, alipokea mamia ya simu kuhusiana na tukio hilo na maoni yake binafsi yalikuwa hivi,

“Tukio la Arizona lilikuwa wazi kabisa kati ya matukio niliyopata kuyaona, tulicho kiona pale ni kitu cha kweli kabisa. Tayari wako hapa viumbe kutoka sayari nyingine”, alisema Davenport.

Miezi mitatu baada ya tukio, Juni 18, 1997 tukio hilo lilianza kuzungumziwa kwenye vyombo vikubwa vya habari duniani na kuanza kupata mvuto na kuvuta hisia za watu. Liliripotiwa kwenye NBC, MSNB, CNN na ABC.

Barani Afrika, tukio la kuonekana kwa UFOs liliwahi kuripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari vichache nchini Zimbabwe, Mwandishi Cynthia Hind aliandika kuwa mnamo tarehe 14 Septemba Ruwa, Zimbabwe vilitua vitu ambavyo vinafanana na UFOs katika shule moja na tukio hilo lilishuhudiwa na wanafunzi wenye umri mdogo (kati ya 5-12) ambao walikuwa wakicheza nje ya uwanja wa shule kipindi walimu wao wakiwa kwenye Mkutano, na siku mbili baada ya tukio hilo (yaani 16 September, 1994) Mwandishi huyo akaamua kuwafanyia usaili wale watoto wote wa shule kwa kuwaambia wachore kitu ambacho walikiona siku ya tukio, huku kila mtoto akiwa peke yake waliweza kuchora mfano wa kitu walichokiona na hapo ndipo wale watoto wakachora michoro ambayo iliweza kufafana jambo hilo lilimfanya mwandishi huyo kubaini kuwa ni UFOs ilitua katika eneo hilo na huku ikiwa imefuatana na vitu vingine vinne.

Kwa takribani miaka hamsini sasa tangu Serikali mbalimbali duniani na watafiti walipoamua kulishughulikia suala la UFOs na kutafuta majibu ya maswali kuhusiana na asili yake hasa ni nini na tija au madhara yake kwa binadamu waishia katika sayari ya Dunia ni yapi lakini hakuna kati ya hao waliokuja na majibu ya kuridhisha ama majibu rasmi kuhusiana na suala la hilo.

Basi kama UFOs zitakuwa ni kweli zipo, na asili yake hasa ni kutoka nje aidha ya sayari yetu ama galaxy yetu, ukweli huo hakuna shaka utakuwa ni changamoto ya namna yake kwa binadamu wote na Kwa upande mwingine ikiwa UFOs ni si kama hivyo tunavyoambiwa ama si hivyo inavyoelezewa na wale walio wahikushuhudia , basi vyombo hivyo vitakuwa ni ushahidi tosha wa mpango kabambe ambao mabilioni ya binadamu hawafahamu hatima na malengo yake ni nini na ambao athari yake huenda ikamuathiri kila binadamu aliyepo kwenye sayari hii.

Na Benedict Liwenga (Maelezo)

Share:

Leave a reply