MAKALA: Sera ya elimu bila malipo inahitaji ufafanuzi wa kina kwa wananchi

298
0
Share:

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imeingia mwaka wa tatu tangu iingie madarakani Novemba 2015. Katika mwaka wa tatu huu wa uongozi wa Rais John Magufuli, inaadhimisha mwaka wa tatu tangu sera ya elimu bila malipo ilipoanza utekelezwaji wake Januari 2016. Sera ya elimu msingi bila malipo inawanufaisha moja kwa moja wanafunzi kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne.

Tangu kuanza kwa utekelezaji wa sera ya elimu msingi bila malipo kumekuwa na mwamko mkubwa wa wazazi na walezi kupeleka watoto wao shuleni hasa wa darasa la kwanza na wale wanaochaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa kidato cha kwanza. Mwamko huo unatokana na serikali kuondoa ada na michango mbalimbali iliyokuwa ikilipwa na wazazi mashuleni.

Kutokana na kuongezeka kasi ya idadi ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, kumepelekea kuzalishwa kwa changamoto mpya. Mathalani kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi mashuleni kutapelekea mahitaji ya majengo mapya, vyoo, walimu wapya, ofisi za walimu, madawati mapya, viti na meza mpya nk.

Shule iliyokuwa na idadi ya wanafunzi 350 huku ikiwa na  madarasa 7, haiwezi kuwahudumia vizuri wanafunzi watakapofika wanafunzi 720 kwa idadi ile ile ya madarasa 7. Hivyo ni dhahiri shule hii itahitaji nyongeza ya madarasa mapya, madawatii mapya ili kuwahudumia wanafunzi 720 waliopo sasa. Kwa muktadha huu inadhihirisha wazi elimu bila malipo imepelekea kuzalishwa kwa changamoto mpya kwa shule nyingi nchini.

Serikali inatumia Shilingi Bilioni 23 kila mwezi kama ruzuku kwa shule zote za msingi na sekondari kufanikisha utekelezaji wa elimu bila malipo. Fedha hizi ni nyingi sana lakini serikali imeona ni vyema kufanya hivi ili kila mtanzania aweze kupata haki ya msingi ya kupata elimu bila kisingizio chochote.

Ieleweke wazi kuwa serikali ilipotangaza sera ya elimu bila malipo ilikuwa imejikita katika michango ile ya moja kwa moja kama ada, michango ya taaluma, mlinzi, karatasi za kufanyia mitihani (ream papers), fedha za mitihani ya mock na Taifa, maji, umeme nk. Changamoto mpya zilizozalishwa na sera hii inahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi wote ili kuweza kutatua changamoto hizi.

Baadhi ya wananchi, baada ya kusikia sera ya elimu bure au bila malipo basi wamejitoa moja kwa moja katika kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini kwa kisingizio kuwa elimu ni bure. Hapa ndipo inapokuja haja ya viongozi wa serikali kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wananchi katika kuwaelimisha wananchi juu ya nini  hasa maana ya “elimu bila malipo”.

Wananchi wakijua dhana ya elimu bila malipo watakuwa wepesi wa kuiunga mkono serikali katika kutatua changamoto za elimu bila malipo. Nimefurahishwa sana na serikali ya kijiji cha Kisemvule kwa kuwashirikisha wananchi wameweza kujenga vyoo vipya 8 katika Shule ya Msingi Kisemvule iliyopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Kama wananchi wa kijiji hiki wangesema elimu ni bure hivyo wasubiri fedha kutoka Halmashauri ya Mkuranga naamini mpaka sasa watoto wao wangekuwa katika adha ya kukosa vyoo.

Miongoni mwa mambo yanayoongeza ufaulu kwa wanafunzi ni uwepo ya chakula shuleni ili wanafunzi wasome wakiwa wameshiba. Mwanafunzi mwenye njaa hawezi kumwelewa mwalimu anapokuwa anafundisha darasani. Wapo wazazi ambao wakiambiwa wachangie mahindi na maharage ili watoto wao wapate chakula shuleni, hawapo tayari kuchangia kwa kigezo cha elimu bure. Nilisikia wananchi wa mkoa wa Njombe wakitoa sababu za mkoa wao kufanya vizuri  na kushika nafasi ya 6 kitaifa katika Mtihani wa Taifa wa darasa la saba 2017.

Sababu mojawapo ya kufanya vizuri kwa mkoa wa Njombe ni wanafunzi kula chakula shuleni. Kama wazazi na walezi wa mkoa wa Njombe wangesema hawachangii chakula kwa kuwa elimu ni bure, watoto wao wasingeweza kufanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba. Najua wazazi na walezi wa mkoa wa Njombe wanajua serikali yao inatoa elimu bila malipo lakini wanajua kama wazazi wanatakiwa kujiongeza katika kuchangia chakula ambacho watakula watoto wao wenyewe.

Mkoa wa Lindi unatarajia kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wapatao 32,000 kwa mwaka huu 2018. Naamini shule nyingi za msingi za mkoa wa Lindi zitakuwa na changamoto ya madarasa na vyoo. Sasa kama wakazi wa mkoa wa Lindi watasubiri serikali imalize tatizo la madarsa, watakuwa hawaitendei haki sera ya elimu bila malipo. Wanatakiwa kujitoa  katika kutoa nguvu kazi na raslimali fedha ili kufanikisha ujenzi wa madarasa na vyoo ili watoto wao wasome katika mazingira mazuri na kupata elimu bora.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda  yupo katika jitihada za kuboresha sekta ya elimu mkoani Dar es Salaam kuhakikisha ujenzi wa ofisi 402 za walimu zinakamilika. Taasisi za serikali, binafsi na wananchi wanajitoa kikamilifu kuhakikisha ofisi hizo zinakamilika.

Ni wajibu wa viongozi wa serikali na kila mwananchi aliyeelewa dhana ya elimu bila malipo kuwaelimisha wengine ili kuboresha elimu yetu. Msisitizo mkubwa unahitajika kutoka kwa viongozi wa juu wa serikali kuwaelimisha wananchi kuhusu elimu bila malipo. Sekta ya elimu inahitaji uwekezaji mkubwa wa raslimali fedha kwa  ushirikiano wa serikali, taasisi binafsi na wananchi. Wananchi wanahitaji kuelewa mipaka ya elimu bila malipo ili pale wanaposhauriwa kuchangia maendeleo ya elimu wawe wepesi kufanya hivyo.

Neno bure au bila malipo lisipotoshwe na kuiachia mzigo wote serikali wa kutatua changamoto zote za elimu. Hii si sawa hata kidogo. Serikali imejitoa kugharamia elimu kwa kutoa ruzuku ya Shilingi Bilioni 23 kila mwezi, wananchi tuunge mkono kutatua changamoto mbalimbali ili wanafunzi wapate elimu bora. Najua watanzania ni waelewa, wapewe elimu kuhusu dhana ya elimu bila malipo ili tuwe na sauti moja katika hili.

Na Reubeni Lumbagala – 0764-666349

Share:

Leave a reply