MAKALA: Taasisi nyingine za malezi ya watoto

107
0
Share:

Katika makala iliyopita, nilichambua taasisi ya familia kama taasisis ya kwanza kabisa katika malezi na maadili bora ya mtoto. Nilieleza kwa undani jinsi wazazi na wanafamilia kwa ujumla walivyo na wajibu mkubwa wa kumtengeneza mtoto kabla taasisi nyingine hazijaonyesha mchango wao.

Malezi na maadili ya watoto ni jambo linalohitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili mtoto akue katika maadili, nidhamu na hatimaye kuwa raia mwema kwa Taifa lake. Katika Makala hii nitaonyesha jinsi taasisi nyingine tofauti na familia zilivyo na nafasi kubwa ya kujenga maadili na malezi bora kwa watoto. Taasisi hizo ni pamoja na :

Moja, Taasisi za kiroho. Hizi ni taasisi za kidini. Dini zote kupitia mafundisho yake zinafundisha mtoto na watu wote kwa ujumla kuwa na maadili mazuri. Mafundisho ya dini yanakazia sana suala la tabia njema, kuwaheshimu wakubwa na wengine, nidhamu, Kuwa na hofu ya Mungu na Kuchukia uovu. Mtoto au kijana aliyelelewa  katika mafundisho ya kiroho atawapendeza wengi wakiwemo wazazi, ndugu, majirani, walimu, viongozi na Mwenyezi Mungu.

Hata matatizo ya kijamii yaliyopo nchini kwetu na duniani kama Uhalifu, Rushwa, Madawa ya Kulevya, Ukahaba, Wizi, ni miongoni mwa mwa matokeo ya kutozingatia mafundisho ya kiroho kutoka kwa viongozi wetu wa dini. Watoto na Vijana wanapaswa kupewa maadili na malezi bora ili kuepukana na matatizo hayo.

Naungana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mwigulu Nchemba wakati wa maadhimisho ya miaka 57 ya Ushirika wa Wanafunzi wa Kiinjili wa Tanzania (Tafes) yaliyokwenda sambamba na kusherehekea miaka 27 ya uwepo wao hapa nchini, alisemma maandalizi ya maadili mema yanaanzia katika ngazi ya familia na taasisi za kiroho. Aliongeza kusema uhalifu wa kikatili ni zao la kutokuwepo kwa hofu ya Mungu kwenye mioyo ya watekelezaji wa matukio ya aina hiyo.

“Tukiwa na watu waliolelewa  katika misingi ya imani, hatutaweza tukapata watu wasiojulikana (Wahalifu) na jambo hili linaniudhi sana, Hatuwezi tukawa na watu wasiojulikana wanaotenda uhalifu na kukimbia kusikojulikana na tutashughulika na nguvu za dola”. Nampongeza Waziri Mwigulu kwa kulitambua hili. Kama watoto na vijana watazingatia mafundisho ya dini vizuri basi tutaisaidia sana hata serikali yetu katika kupambana na matatizo ha kijamii ambayo husababishwa na kutozingatia mafundisho na maadili ya dini.

Mbili,Taasisi za elimu.Walimu pamoja na kuwa na jukumu kubwa la kuwafundisha watoto masomo ya darasani lakini pia wanawajibika kuwalea watoto katika malezi na maadili mema. Ndio maana Mwalimu yeyote ni lazima asomee somo la Saikolojia na Uongozi awapo Chuoni.

Kuanzia shule za Misingi, Sekondari, Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu, watoto na vijana hufundishwa maadili na tabia njema na walimu wao. Kupitia mada zinazofundishwa katika masomo yao, watoto na vijana hujifunza mambo mengi mazuri ambayo kama watazingatia yatawasaidia katika maisha yao ya sasa naya baadae.

Hufundishwa nidhamu, utii wa sheria, kufanya kazi, kuishi kwa ushirikiano, kuepuka tabia mbaya, kuwasaidia wengine, usafi, nk. Mtoto anayezingatia haya anajijengea kesho yake nzuri sana katika maisha yake.

Katika Shule za Msingi na Sekondari wapo Walimu wa madarasa, Walimu Walezi wa Wanafunzi wa Kiume (Patrons) na Walimu Walezi wa Wanafunzi wa Kike (Matrons)  hawa wote wamewekwa kuwa karibu sana na wanafunzi katika kuwalea wanafunzi katika malezi bora.

Katika Vyuo Vikuu wapo Washauri wa Wanafunzi (Dean of Students) ambao wamewekwa ili kuwasaidia wanafunzi kutatua changamoto zao pale wanapohitaji msaada na pia kuwasaidia vijana wa Vyuo Vikuu kuwa na maadili na tabia njema. Walimu hawa kwa kushirikiana na walimu wenzao wanashirikianna katika kupanda mbegu nzuri ya Maadili na Malezi kwa Watoto na Vijana.

Tatu, Serikali. Serikali ina wajibu mkubwa wa kutunga sheria, sera na kuzisimamia ipasavyo ili kuwasaidia watoto na vijana kukua katika maadili na malezi bora. Serikali iwaajibishe wazazi wote wanaoshindwa kuwatunza watoto wao ambao hupelekea watoto na vijana kujiingiza katika vitendo viovu kama ukahaba na wizi.

Sheria zinazotungwa zilenge kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, ndoa za utotoni, manyanyaso na vitendo viovu kama ubakaji vinavyofanywa na wasiopenda maendeleo ya watoto na vijana. Naamini serikali ikifanya hivyo, watoto na vijana watakuwa katika malezi bora ambayo ni chachu ya maendeleo ya Taifa lolote.

Kwa mujibu wa Takwimu za nchi yetu, nusu ya raia ni watoto chini ya miaka 17. Kama kundi hili litapuuzwa na kutelekezwa, basi kama Taifa tutakuwa na kazi kubwa ya kujenga upya nchi yetu katika Malezi na Maadili. Miongozi mwa maeneo muhimu ya uwekezaji katika nchi yetu ni katika Watoto na Vijana. Kwa hiyo Familia, Taasisi za dini, Taasisi za Elimu kwa kushirikiana na Serikali huchangia malezi bora ya watoto na vijana. Tafakari.

Mwandishi wa Makala hii Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0764-666349.

Share:

Leave a reply