Mama Samia kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukaribisha viongozi Dodoma

588
0
Share:

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla maalumu ya kuwakaribisha viongozi wa Serikali itakayofanyika Machi 5  mwaka huu mkoani Dodoma.

Hafla hiyo imeandaliwa na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na
itafanyika mkoani humo katika viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) kuanzia  saa 8 kamili mchana.

Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Jeremia Mwakyoma ameyasema  hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  maandalizi ya ujio wa viongozi hao katika Mkoa huo.

Mwakyoma amesema viongozi wa Serikali kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi ni  sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo Mkoa  utawakaribisha rasmi Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu  Makatibu Wakuu wa Wizara waliohamia kutoka Jijini Dar es Salaam.

“Tukio la viongozi wa Wizara kuhamia Makao Makuu Dodoma ni la kihistoria  ndio maana uongozi wa Serikali ya Mkoa umeona ni vema kuweka utaratibu  rasmi wa kuwakaribisha viongozi hao,” alisema Mwakyoma.

Afisa Habari Mwakyoma amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa huo pamoja na  Mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye hafla hiyo.

Mnamo Julai 25 mwaka 2016 katika maadhimisho ya siku ya mashujaa
yalioadhimishwa mkoani Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt,  John Pombe Magufuli alitangaza rasmi Serikali kuanza mchakato wa kuhamia  Dodoma ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Nchi.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Share:

Leave a reply