Mambo matano muhimu aliyozungumza Rais Magufuli katika Mkutano na Wazee wa Dar

1493
0
Share:

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo jumamosi, Februari 13 amefanya mkutano na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee na kutoa hutuba ambayo ilikuwa ikionyesha ni kipi amekifanya ndani ya siku 100 tangu alipoingia madarakani.

Pia alizungumzia mipango mbalimbali iliyopo kwenye serikali yake ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maisha bora kwa kutumia vizuri maeneo ambayo serikali inayaona kuwa na makusanyo mazuri na kuwapunguzia mzigo masikini ambao ndiyo walikuwa wakinyonywa zaidi hapo awali.

Mo Dewji Blog imekuandalia mambo matano muhimu ambayo Rais Magufuli ameyazungumza katika mkutano huo na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

IMGS4067

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Naibu Spika wa Bunge Dkt.Tulia Ackson wakati Rais John Magufuli alipozungumza na Wazee wa Dar es salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam Februari 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Rais Magufuli amemaliza maneno yaliyokuwepo kuwa kwanini yeye kama Rais wa Tanzania haingilii ili kumaliza tofauti zilizojitokeza visiwani humo.

Alisema yeye kuwa rais wa Tanzania haina maana kuwa anaruhusiwa kuingilia uchaguzi wa visiwani humo na hakuna kifungu cha kisheria kinachomruhusu kuwa na maamuzi katika uchaguzi wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) ni kama tume zingine duniani za uchaguzi na zinatakiwa kuwa huru katika kufanya kazi hivyo kama kuna watu au chama kinadhani anaweza kuingilia uchaguzi wa Zanzibar hawezi na hata  fanya hivyo.

Pia alielezea majukumu yake na kusema kazi yake ni kuhakikisha kunakuwa na usalama na kama kuna watu watataka kusababisha kupotea kwa amani visiwani Zanzibar vyombo vya usalama vipo na vitawashughulikia wote watakao sababisha upotevu wa amani.

IMGS4114

Rais John Magufuli akiteta na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Mkutano kati yake na wazee wa Dar es salaam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam Februari 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kazi ya kutumbua majipu, Rais Magufuli ameonyesha nia ya dhati ya kuendelea kuwachukulia hatua watumishi wote ambao wanaonekana kuhusika katika kukwamisha maendeleo ya taifa na kupitia serikali yake atahakikisha wote waliohusika wanafikishwa mbele vya yombo vya sheria ili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika hilo aliwaomba Watanzania kuendelea kushirikiana na serikali ili waweze kufanya kazi ambayo wananchi waliwaagiza wawafanyie pindi watakapopata nafasi ya kuingia madarakani.

Pia alizungumzia kuhusu kasi ya utendaji wa kazi uliopo mikoani na kueleza kuwa kwa sasa ni wasaa wa wakuu wa mikoa nchini kujipima uwezo wa kama wanaweza kufanya kazi kwa kasi anayoitaka kabla hajatangaza wakuu wa mikoa atakaofanya nao kazi.

Kusaidia upatikanaji wa huduma bora za kijamii kama Afya na Elimu, Kwa kutambua matatizo waliyonayo Watanzania katika huduma za kijamii, Rais Magufuli ameendelea kuonyesha Watanzania kuwa ana nia ya kweli na kuwasaidia wananchi wake.

Kwa kuonyesha kuwa hatanii katika hilo Dkt. Magufuli amemwagiza Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu siku mbili kuhakikisha anasimamia tatizo la wodi wa wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili linamalizika na wanakuwa na vitanda vya kutosha.

Pia alimuahidi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa,. Sadiki Meck Sadick kuwa atampatia bilioni mbili ili kumaliza changamoto za elimu bure ambazo zimejitokeza na zingine milioni 100 akiwa amechanga yeye, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Manaibu Waziri.

IMGS4133

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wazee wa Dar es salaam kabla Rais John Magufuli hajazungumza nao kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam Februari 13, 2016.

Kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam, Kwa kutambua kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha Tanzania, Rais Magufuli ameonyesha kuwa na mipango mingi ya kuufanya muonekano wa jiji la Dar unakuwa mzuri na wenye urahisi wa watu kufanya shughuli zao.

Baadhi ya mipango ambayo aliisema ni ujenzi wa barabara ya juu kutoka kwenye ufukwe wa Coco hadi Hospitali ya Agha Khan ambayo itapita juu ya maji, ujenzi wa barabara za juu katika maeneo yaliyo na msongamano mkubwa wa magari, utanuzi wa barabara na upatikanaji wa huduma bora za kijamii.

Nafasi ya vyombo vya habari, Rais ameonyesha kusikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinaonekana kuandika habari ambazo zinaweza kupelekea upotevu wa amani nchini.

Pia amevisifia baadhi ya vyombo vya habari ambavyo ameona kuwa vinaandika habari ambazo haziwezi kusababisha upotevu wa amani nchini na kuahidi serikali kuendelea kufanya kazi pamoja na vyombo vya habari ila akivitaka kuandika habari njema kwa watanzania na kuisaidia serikali kuyasema maovu ili wao wawachukulie hatua wahusika.

Share:

Leave a reply