Manara amtumia salamu Malinzi, aomba serikali iingilie kati sakata la Kagera Sugar

3506
0
Share:

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara ameiomba Serikali na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kuingilia kati sakata la Simba dhidi ya mchezaji wa timu ya Kagera Sugar, Mohamed Fakhi anayedaiwa kucheza mechi ya Simba ilhari ana kadi tatu za njano kinyume na taratibu na kanuni za TFF.

Manara ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari, ambapo ametuhumu baadhi ya viongozi wa TFF kuwa na njama za kuihujumu klabu hiyo, huku akivitaka vyombo vya dola ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ichunguze sakata hilo.

“Kilichojiri ndani ya TFF juu ya udharimu, hujuma, upendeleo kwa baadhi ya timu nyingine dhidi ya Simba hakikubaliki kabisa na msimamo wetu tunataka tuombwe radhi kwa kuhusishwa na tuhuma za kufoji email, tuna hakika kwa asilimia mia hatujafanya hivyo njama zote hizi ni kutaka kuibeba Yanga,” amesema.

Hata hivyo, Manara amemtumia salamu Rais wa TFF kwa kusema kuwa Jamali Malinzi mwisho wake umefika na kudai kuwa haofii kufungiwa na shirikisho hilo kutokana na uamuzi wake wa kusema ukweli kwa ajili ya kutetea klabu hiyo.

“Serikali na TFF wafanye uchunguzi wenyewe hata Malinzi akitaka kunifungia anifungie miaka milioni kwa hili tumechoka kuonewa. Malinzi asipochukuliwa hatua hadi Jumatatu tutamwaga mboga. TAKUKURU ifanye kazi yao kama kinachofanyika ni haki sawa. Malinzi sasa imefika mwisho wake,” amesema na kuongeza.

“Msimamo wa Simba tunataka haki itendeke, kama Malinzi na timu yake wamejipanga kuidhurumu Simba patakua hapatoshi nchi hii.”

Na Regina Mkonde.

Share:

Leave a reply