Mauzo ya Hisa DSE yapanda na kufikia Trilioni 19.7

572
0
Share:

Kufuatia kuongezeka kwa bei za hisa za KCB (8%), ACACIA (5.5%), na TBL (4.3%).Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) umepanda kwa takribani Shilingi Bilioni 500, kutoka Shilingi Trilioni 19.2 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 19.7 wiki iliyoishia tarehe 17 Machi 2017. 

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Afisa Masoko Mwandamizi wa DSE, Marry Kinabo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo ameeleza kuwa,  mtaji wa kampuni za ndani umepanda kwa takribani shilingi Bilioni 90, kutoka Shilingi Trilioni 7.4 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 7.5.

“Hali kadhalika idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa imeongezeka kutoka hisa 640,000 hadi hisa Milioni 3 thamani ya mauzo ya hisa yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 1.3 wiki iliyopita hadi Shilingi Bilioni 32 wiki iliyoishia tarehe 17 Machi 2017,” amesema Kinabo.

Katika hatua nyingine, amesema mauzo ya hati fungani katika wiki iliyoishia  Machi 17, 2017 yameongezeka kwa Shilingi Bilioni 21.5 kutoka thamani ya Shilingi Milioni 113 wiki iliyopita hadi Shilingi Bilioni 21.6, kutokana na mauzo ya hati fungani nane (8) za serikali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 30 kwa jumla ya gharama ya Shilingi Bilioni 21.6.

Kwa upande wa viashiria, amesema kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko kimeongezeka kwa pointi 54 kutoka pointi 2,212 hadi pointi 2,266 kutokana na kuongezeka kwa bei za hisa za kampuni mbali mbali zilizopo sokoni. Wakati Kiashiria cha kampuni za ndani  kimeongezeka kwa pointi 43 kutoka pointi 3,525 hadi pointi 3,568 kutokana na kuongezeka kwa bei za hisa za kampuni mbali mbali za ndani.

“Sekta ya viwanda (IA) wiki hii imeongezeka kwa pointi 81 kutoka pointi 4,534 hadi pointi 4,615 kutokana na kuongezeka kwa bei za hisa za TBL kwa asilimia 4.3% kutoka Shilingi 11,500 hadi Shilingi 12,000,

“Sekta ya huduma za kibenki na kifedha (BI) wiki tajwa imebaki kwenye wastani wa pointi 2,541.Sekta ya huduma za kibiashara (CS) wiki husika imebaki kwenye wastani wa pointi 3,137.” amesema.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply