Mbunge Kadutu aliongeza Baraza la Madiwani Kaliua

465
0
Share:

Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu wilayani Kaliua Mkoani Tabora, John Kadutu amewapongeza Wenyeviti wa Kamati ndogo za baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kwa uwezo wao mkubwa wa kufafanua miradi ya maendeleo inayotekelezwa.

Pongezi hizo zimetolewa  katika kikao cha kufunga mwaka cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Kaliua.

Alisema licha ya kuwa Wenyeviti wa kamati hizo ni madiwani wanaowakilisha kata zao na baadhi yao hawana hata elimu ya kutosha, lakini wako makini sana na uelewa wao wa miradi uko juu.

Aliwasifu madiwani hao kwa kufuatilia na kuhoji ufanisi wa miradi yote inayotekelezwa na hata pale wanapohitaji ufafanuzi majibu yanayotolewa na Wenyeviti wa kamati hizo yanafafanua vizuri na kutoa majawabu stahiki.

Kadutu alisema Wenyeviti wa kamati wako makini sana hata kuliko Wataalamu wenyewe wa halmashauri, huku akibainisha kuwa wakati wa mijadala baadhi ya wataalamu hawafuatilii kwa umakini na hata kufafanua zaidi wengine hawawezi.

Aliongeza kuwa Wakuu wa idara na Wataalam wa halmashauri hiyo wanapaswa kuwa na ufahamu mpana wa miradi inayotekelezwa na uwezo wa kujieleza au kuhamisha uelewa wao ndani ya fahamu za madiwani.

“Hapa tatizo kubwa la wataalamu wetu wa idara ni kukosa umakini na kutofuatilia kwa kina mijadala na hoja zinazotolewa na waheshimiwa madiwani, ndugu zangu kuweni makini sana,” alisema.

Aidha Kadutu alishauri Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Haruna Kasele na madiwani wote kudumisha utulivu, mshikamano na ushirikiano na watalaamu wa halmashauri ili kuwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kimaendeleo katika wilaya hiyo.

Alisema kazi ya diwani ni kushauri, kusimamia na kufuatilia utekelezaji miradi ya maendeleo katika halmashauri ikiwemo kutetea maslahi ya watumishi au kuchukua hatua stahiki, vivyo hivyo kwa wakuu wa idara kwani wanapaswa kutoa ushirikiano wa karibu zaidi kwa madiwani.

Aidha alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo John Pima kushirikiana na madiwani hao na kuhakikisha haki zote zinazowapasa zinapatikana ili kuendelea kudumisha utulivu na amani.

Alishauri kuendelea kufuatwa kwa mwongozo, kanuni na taratibu za uendeshwaji wa vikao vya baraza la madiwani ili kudumisha utulivu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa madiwani na wataalamu wa halmashauri.

Na Mussa Mbeho, Kaliua

Share:

Leave a reply