Meli ya Hospitali kutoka China yawasili Dar, kuanza kutoa huduma Novemba 20

343
0
Share:

Meli kubwa ya Jeshi la Jamhuri ya China yenye hospitali (Chinese Hospital Ship) imewasili katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na madaktari bingwa 381, vifaa na madawa ya kutosha kwaajili ya kuanza kwa zoezi la upimaji na matibabu bure kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ametembelea Meli hiyo na kujionea namna imesheheni vifaa tiba vya kisasa ambapo ndani yake vipo vyumba 8 vya upasuaji, vyumba vya ICU, wodi za wagonjwa, vyumba vya madaktari, mitambo ya kisasa, maabara na sehemu ya wagonjwa kupumzika.

Meli hiyo ya kipekee ina helkopta kwaajili ya wagonjwa ambapo kwa ulimwenguni meli za aina hiyo zipo mbili pekee ambapo moja ni hii iliyokuja Tanzania na nyingine ipo Nchini Marekani.

RC Makonda amesema Meli hiyo ina mfumo maalumu wa Mawasiliano Kati ya Meli na Taifa la China pale inapotokea Ugonjwa umeshindikana.

Tayari Jopo la wataalamu 30 wameenda Hospital za Amana, Temeke, Mwananyamala na Ocean Road kwaajili ya kukarabati na kufunga vifaa vipya kwa vile vitakavyobainika vilivyoharibika au kufa.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha hakuna mwananchi anaepoteza maisha kwa kigezo cha kukosa huduma.

Amewasihi wananchi wenye magonjwa yaliyoshindikana kwa muda mrefu kuchangamkia fursa hii ya matibabu bure chini ya madaktari bingwa kutoka China.

Kwa upande wake kiongozi mkuu wa meli hiyo Kamanda Guan Bailinamesema wamekuja na vifaa vya kutosha na madaktari waliobobea hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi.

Share:

Leave a reply