Mimba zapunguza idadi ya wanafunzi wa kike mashuleni wilayani Nyang’hwale

299
0
Share:

Zaidi ya wanafunzi 35 wa Shule za msingi na Sekondari wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita wamekatishwa masomo kutokana na kupatiwa ujauzito katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Carlos Gwamagobe amesema licha ya mimba hizo kuripotiwa katika kituo cha Polisi mkoani humo lakini hakuna mtuhumiwa aliyehukumiwa kutokana na kusababisha ujauzito.

“Kwasasa natangaza hivi mtoto yeyote atakaebainika kuwa ni mjamzito atafungwa kuanzia wazazi wake, aliyempatia ujauzito na binti mwenyewe hii naamini itasaidia kupunguza vitendo hivi,” alisema Gwamagobe.

Hata hivyo MO Blog ilifika katika familia ya Zakayo Nganiko  yenye mwanafunzi  anayesoma darasa la saba shule ya msingi Bukwimba anaesadikiwa kupatiwa ujauzito na mwalimu wake wa somo la hesabu ili kupata kisa hicho kwa kina.      

“Ilikuwa mwezi wa pili mwaka huu Mwalimu wangu wa hesabu aliniambia niende nyumbani kwake nikamsaidie kuosha vyombo ndipo aliponiambia nifuate vyombo chumbani kwake nikakata akawa amevifuata mwenyewe siku ya pili tena akaniambia nikaoshe vyombo nikaenda ndipo aliponivuta hadi chumbani kwake na kunifanyia kitendo hicho tulipomaliza kufanya hivyo alinipatia shilling elfu tano nikarudi shule,” alisema mwanafunzi aliyepatiwa ujauzito.

Wazazi wa msichana huyo wamesema kesi hiyo hata mwalimu mkuu wa shule hiyo aliitambua ila ameamua kuifumbia macho kinyume cha sheria.

Kwa upande wake mwalimu wa somo la hesabu anayetuhumiwa kumpatia ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba amekana kutenda kosa hilo.

“Mimi sihusiki kabisa na ujauzito huo kwani sijawahi kumfanyia chochote binti huyu pengine wamuulize vizuri ujauzito ni wa nani lakini sio mimi,” alisema Mwalimu wa Hesabu.

Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Bukimba, Kabumu Kafumba  amekiri kuwa mwanafunzi huyo ana ujauzito na kudai kuwa hatambui kama ujauzito huo ni wa mwalimu huyo ama laa na kuongeza kuwa vipimo vya daktari pindi vitakapobaini atafikishwa katika vyombo vya dola. 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Hamim Ngwiyama ameahidi kulivalia njuga suala hilo  huku akiomba wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.

Mkuu wa wilaya amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kuachana na vishawishi vinavyoweza kukatiza ndoto zao.

 Na Veronica Martine, Geita

Share:

Leave a reply