Mjane amueleza Rais Magufuli jinsi mahakama za Wilaya zinavyoshiriki kudhurumu mirathi

2057
0
Share:

Katika hali isiyo ya kawaida baada ya Rais John Magufuli kuhutubia katika maadhimisho ya siku ya sheria na mwaka mpya wa mahakama, mjane aliyefahamika kwa jina la Swabaha Mohammed Shosi amevamia katika maadhimisho hayo kwa lengo la kutoa malalamiko ya kudhurumiwa mirathi yake na Wakili wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga, Alfred Akaro kwa kushirikiana na mtoto wa Marehemu mumewe Saburia Mohamed Shosi.

Baada ya Mjane huyo kutoa malalamiko yake ambapo alidai kuwa wahusika kila mara humtumia jumbe za vitisho ikiwemo za kutaka kumuua ili asifuatilie mirathi yake, Rais Magufuli aliwaagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka DPP Biswalo Mganga, kuishughulikia kesi hiyo pamoja na kumpa ulinzi ili asidhurike.

Awali Swabaha alimueleza Rais Magufuli kuwa mtoto wa nje ya ndoa wa marehemu mume wake Saburia Mohammed Shosi, kwa kushirikiana na wakili wa mahakama ya wilaya Tanga Alfred Akaro wamefoji wosia wa mume wake Mohamed Shosi kwa lengo la kumdhurumu mirathi aliyoiacha.

Swabaha alidai kuwa, licha ya kushinda katika kesi ya mirathi aliyoifungua mwaka 2010, mahakama ilishindwa kumpa haki yake badala yake wahusika waliishinikiza mahakama hiyo kumfungulia mashitaka saba.

Alisema, suala lake alilifikisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka DPP Biswalo Mganga, na kwamba bado halijatafutiwa ufumbuzi.

“Wakili wa serikali kwa kishirikiana na mtoto wa marehemu wamefoji usia wa marehemu mume wangu, na msimamizi wa mirathi waliyemuweka hausiki ni mpangaji hata hivyo wanawake waliowekwa katika wosia huo kama wake ni mahawara,” alisema.

Swabaha amesema kuwa, wajane wengi hudhurumiwa haki zao hasa za mirathi kutokana na baadhi ya watumishi wa mahakama hasa za wilaya kukosa uaminifu kwa kushirikiana na wahalifu kudhurumu haki za wanyonge kwa lengo la kujipatia pesa.

Share:

Leave a reply