Mkemia Mkuu atoa tamko kuhusu Techno Net Scientific kukutwa na Kemikali Bashirifu bila kibali

844
0
Share:

Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyp chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imetoa ufafanuzi kuhusu kampuni ya Techno Net Scientific  Ltd  iliyokutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili/kibali kutoka Mamlaka hiyo.

Akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo  19 Mei 2017, Jijini Dar es Salaam, Mkemia Mkuu wa Serikali  Prof. Samwel  Manyele  amebainisha kuwa  wao walitoa usajili wa muda wa miaka miwili na ulishakwisha tokea mwezi Aprili 2016, hivyo kwa hatua ya kukutwa na Kemikali hiyo kwa sasa suala hilo linashughulikiwa na vyombo husika ilikuchukua hatua zaidi, ameeleza Mkemia  huyo, Prf. Manyele.

Aidha, Prf. Manyele amefafanua kuwa: Taarifa za  kampuni  ya Techno Net Scientific Ltd  inayojihusisha na uingizaji  na uuzaji wa kemikali nchini  zikiwemo kemikali bashirifu kwenye viwanda, maabara za shule, vyuo vikuu, taasisi za uchunguzi na utafiti na hospitalini nchini walipatiwa usajili wa muda wa miaka miwili (2), wenye namba  ya usajili 9331-94–0046 mnamo 30 Aprili, 2014 hata hivyo usajili ambao muda wake wa usajili ulikwisha 30 Aprili 2016.

“Baada ya muda wa usajili kuisha kampuni hii iliwasilisha maombi ya kuhuisha usajili wake ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti cha usajili kitakapopatikana.

Hata hivyo, kampuni hiyo iliendelea na shughuli za kemikali pamoja na kuwa muda wa cheti cha usajili umekwisha. Aidha,  kuna taarifa kuwa kampuni hii imekuwa ikiingiza kemikali nchini kwa kutumia njia za udanganyifu ikiwa ni pamoja na kutumia vibali vya bandia” Alieleza Prf. Manyele.

Prf. Manyele ameongeza kuwa,  Kufuatana na taarifa mbalimbali za kufanya kazi kinyume cha Sheria, mamlaka za usimamizi ikiwa ni pamoja na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa zilifanya ukaguzi wa pamoja na taarifa ya pamoja ya ukaguzi huo, imepelekea vyombo vya dola kuanzisha uchunguzi kuhusiana na shughuli za kampuni hiyo.

Aidha,  taratibu za uchunguzi zitakapokamilika, kampuni hiyo itafikishwa mahakamani.

Awali, imeelezwa kuwa, kampuni hiyo ya Techno Net Scientific Ltd ilikutwa na Lita 6494 za kemikali bashirifu zenye uwezo wa kuzalisha aina mbalimbali za dawa za kulevya .

Ilielezwa kuwa, Kemikali bashirifu zenye uwezo wa kuzalisha aina mbalimbali za dawa za kulevya zlizoingizwa nchini kwa vibali vya kughushi na kuhifadhiwa na kampuni hiyo ya  Techno Net Scientific iliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam  na kwa sasa uchunguzi bado unaendelea.

Hata hivyo Mkemia huyo amebainisha kuwa, kampuni hiyo ilikutwa na baadhi ya Maghala yake ikiwemo Bagamoyo na Mkoani Kilimanjaro  ambapo wao hawakuwa na taarifa ya maghala hayo hali ambayo ni kinyume na sheria zilizowekwa ambayo ni sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015 inayosimamiwa na mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na sheria ya usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani namba 3 ya mwaka 2003 inayosimamiwa na Mkemia  huyo wa Serikali.

Mkemia Mkuu wa Serikali  Prof. Samwel  Manyele (wa tatu kutoka kushoto) akizungumza mapema leo 19 Mei-2017, ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Wengine ni maafisa wa watendaji wakuu wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyp chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Baadhi ya Maafisa  na watendaji wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyp chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakifuatilia mkutao huo na waandishi wa Habari.

Mkutano huo ukiendelea

Mkemia Mkuu wa Serikali  Prof. Samwel  Manyele akizungumza mapema leo 19 Mei-2017, ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Wengine ni maafisa wa watendaji wakuu wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyp chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Nyumba ya Mkemia Mkuu wa Serikali (Mkemia House) iliyopo Jijini Dar es Salaam ambayo ni ofisi Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyp chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Picha zote na Andrew Chale).

Share:

Leave a reply