Mradi wa Gonga Kengele kwa Ajili ya Usawa wa Kijinsia wazinduliwa nchini

199
0
Share:

Mpango wa kimataifa unaoshirikisha masoko ya hisa zaidi ya hamsini ulimwenguni, ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake hapa nchini -UN Women Tanzania kwa kushirikiana na mtandao wa UN Global Compact Network Tanzania wenye lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia kwenye sekta ya uchumi, umezinduliwa kwa mara ya kwanza kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). 

Mpango huo wenye kauli mbiu ya ‘Gonga Kengele kwa Ajili ya Usawa wa Kijinsia’ ulizinduliwa leo Machi 8, 2018 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Sihaba Nkinga katika hafla ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika katika Ofisi za DSE.

Akizungumza katika hafla hiyo, Nkinga amezitaka sekta binafsi pamoja na kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam kuongeza juhudi zao katika kukuza usawa wa kijinsia, hasa kwenye nafasi za kazi, uwekezaji na uvumbuzi wa masuala mbalimbali kwa kuwa mambo hayo ni muhimu katika kujenga uwezo wa wanawake kiuchumi.

Naye Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa –UNDP, Alvaro Rodriguez akizungumza katika hafla hiyo, amesema kama jamii ya kimataifa inataka kutekeleza malengo 17 ya maendeleo endelevu- SDG’S bila ya kumuacha mtu nyuma, zinahitajika hatua za haraka kumaliza tofauti za usawa wa kijinsia pamoja na kuwezesha wanawake kiuchumi hasa kwenye sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Moremi Marwa soko hilo limeungana na masoko ya mitaji zaidi ya 50 ulimwenguni ili kugonga kengele kwa jamii kuhusu usawa wa kijinsia ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika biashara na maendeleo endelevu.

Share:

Leave a reply