Mradi wenye lengo la kumsaidia mama mjamzito na mtoto wazinduliwa

232
0
Share:

Naubu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa wadau wa sekta ya afya na watoa huduma za afya hasa wauguzi na wakunga wanatakiwa kujikita zaidi kwenye kuokoa na kuboresha afya ya mama mjamzito na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Akizungumza hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa Ukunga salama (More and Better Midwives) uliofanyika leo katika Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bukumbi kilichopo Wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

“Sisi sote tunafahamu umuhimu wa wauguzi na wakunga katika kuimarisha afya ya mama na mtoto hivyo Serikali ya awamu ya tano tumejipanga kuhakikisha kuwa tunapunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama na mtoto,” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali inafahamu kuna changamoto ya upungufu wa watumishi katika kada mbalimbali za afya pamoja na nyinginezo na wanaendelea kuzifanyia kazi ikiwa kutoa kipaumbele cha ajira za wauguzi na wakunga.

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amewaonya wakunga na wauguzi wenye tabia ya kutumia lugha chafu kwa wagonjwa pamoja na kuacha vitendo vya kuwaomba rushwa kwani fani hiyo inaendeshwa kwa taaluma na maadili.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Misungwi Bw. Juma Sweda amesema kuwa wananchi wa Wilaya hiyo wanatakiwa wawe mstari wa mbele katika kukata bima za afya kwani husaidia kuokoa gharama nyingi pindi wanapopata maradhi na mpaka hivi sasa wananchi wenye bima ta afya inakadiriwa ni 9100.

Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Ukunga Salama nchini Dkt. Julius Masanika amesema kuwa mradi huo utafadhili wanafunzi wa kanda ya ziwa na kanda ya magharibi wanaojiunga na vyuo vya Uuguzi na Ukunga wasio na uwezo kwa kuwalipia ada pamoja na mahitaji mengine.

Kwa upande wake Mwanafunzi wa Uuguzi na Ukunga katika Chuo cha Bukumbi ambaye anafadhiliwa na mradi huo Rose Julius amesema kuwa anawasihi wanafunzi wafanye bidii kwenye masomo ya sayansi na hatimae wachukue fani ya uuguzi na ukunga katika kukabiliana na changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi.

Mbali na ufunguzi huo wa mradi wa Ukunga salama unaojulikana kama “More and Better Midwives” ambao umeshirikisha taasisi isiyo ya Kiserikali JHPIEGO, wawakilishi kutoka Chama cha wakungwa Canada(CMA) na Chama cha wakungwa Tanzania TAMA pia alitembelea Zahanati ya Kambi ya wazee Bukumbi, Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure ili kujua hali ya upatikanaji wa dawa .

Share:

Leave a reply